23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Airpay Tanzania yadhamini Tamasha la Pili la Fahari ya Zanzibar

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Kampuni ya Airpay Tanzania imetangaza udhamini wake katika tamasha la pili la Fahari ya Zanzibar, linalotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 20 hadi 27, 2024, kwenye Viwanja vya Dimani Fumba, Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, anatarajiwa kuzindua tamasha hilo.

Akizungumza leo, Septemba 13, 2024, na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Airpay, Yasmin Chali, alisema kampuni hiyo ni mmoja wa wadau wakuu wa tamasha hilo. Airpay inatoa huduma za kidijitali zenye lengo la kurahisisha malipo ya kifedha kwa watu wa kawaida, wafanyabiashara, na wajasiriamali wadogo.

“Tumefurahi kuwa sehemu ya Tamasha la Pili la Fahari ya Zanzibar 2024, ambalo linaonyesha ukuaji wa sekta ya ujasiriamali Zanzibar. Ushirikiano wetu na Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, pamoja na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), unalenga kuimarisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali na huduma nyingine za kifedha kwa wajasiriamali,” alisema Chali.

Chali aliongeza kuwa Airpay inatambua na kuthamini jitihada za Serikali ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi, katika kuweka mazingira bora kwa wajasiriamali kuanzisha na kukuza biashara zao. Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Airpay na serikali utachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar.

“Kwa niaba ya timu ya Airpay, tunampongeza Rais Mwinyi kwa jitihada zake za kuleta mazingira rafiki kwa wajasiriamali na wananchi kwa ujumla. Pia tunatoa shukrani kwa ZEEA kwa ushirikiano unaoendelea kuhakikisha mifumo yetu ya kifedha inawafikia wajasiriamali na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Zanzibar,” alisema Chali.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif, alisema tamasha hilo litatoa fursa kwa wajasiriamali wa Zanzibar kutambulika zaidi katika masoko ya kimataifa na kusaidia kukuza bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Tamasha hili litawapa wajasiriamali wetu nafasi ya kubadilishana uzoefu na wajasiriamali kutoka nje ya nchi, hivyo kusaidia kukuza biashara zao katika ngazi ya kimataifa,” alisema Waziri Sharif.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan Mohamed, aliwataka wajasiriamali wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tamasha hilo, akibainisha kuwa ni fursa kubwa kwao kuonyesha bidhaa zao na kupata masoko mapya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles