23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yalaani mauaji ya Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema, yataka uchunguzi wa haraka

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesikitishwa na tukio la mauaji ya Mjumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ali Kibao, na kusisitiza kuwa kinalaani vikali tukio hilo huku kikiunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha uchunguzi unafanyika haraka na watakaopatikana kuhusika wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza leo, Septemba 13, 2024, jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema chama hicho kinataka kuona waliohusika na mauaji hayo wanapatikana kwa gharama yoyote. Aidha, alisema kama Serikali itaona kuna ulazima wa kuleta wachunguzi kutoka nje ya nchi, CCM itaunga mkono hatua hiyo kwani lengo ni kuona wahusika wanachukuliwa hatua stahiki.

“Kama mnavyofahamu, siku chache zilizopita ndugu Ali Mohamed Kibao alitekwa na baadaye kuuawa. Chama chetu kinasikitishwa sana na tukio hili. CCM inapinga vikali vitendo vya mauaji kama haya na tumeendelea kusisitiza kwamba nchi yetu imejengwa juu ya misingi ya amani, umoja, na mshikamano,” alisema Dk. Nchimbi.

Aliongeza kuwa nchi inapitia changamoto kubwa, lakini CCM inasisitiza umuhimu wa kuliwezesha Jeshi la Polisi kufanya kazi zao kikamilifu kwa mujibu wa ilani ya chama kipengele cha 105k.

Dk. Nchimbi pia alizungumzia tamko lililotolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kuhusu kutoa amri kwa Serikali kuwataja waliohusika na mauaji hayo kabla ya Septemba 23, 2024, vinginevyo wao watachukua hatua.

“Mtu kama Mbowe anaweza kutoa amri kwa Rais? Ukiona mtu anafikia hatua ya kutoa tamko kama hilo, ni wazi kuwa kuna njama kubwa ya kuvuruga amani nchini. Ni kazi yetu sisi, CCM na wapinzani, kushirikiana kuhakikisha kundi hili la watekaji linashughulikiwa ipasavyo,” aliongeza.

Dk. Nchimbi alisisitiza kuwa Rais Dk. Samia yupo madarakani kwa mujibu wa Katiba na haiwezi kuondolewa kwa kauli kama “Samia Must Go” zilizotolewa na Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA).

“Ndio maana tuna uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano, ambapo wananchi huwachagua viongozi wao kwa njia ya kidemokrasia. Hakuna kitu kama ‘Samia Must Go’. Rais Dk. Samia ataendelea kuongoza kwa mujibu wa Katiba yetu.”

Akizungumzia suala la Jeshi la Polisi, Dk. Nchimbi alieleza kuwa kumekuwa na juhudi za kujaribu kufarakanisha jeshi hilo na wananchi, lakini CCM inaendelea kuona mafanikio ya ushirikiano kati ya jeshi hilo na wananchi.

“Kati ya mwaka 2017 na 2023, tumeshuhudia polisi 141 wakijeruhiwa katika matukio ya uhalifu yanayohusisha majambazi. Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa kuhakikisha amani inatawala, na haikubaliki kuona matukio machache yanataka kulivuruga jina zuri la jeshi hilo,” alisema.

Kuhusu watu waliopotea, Dk. Nchimbi alisema, “Kwa miaka mitano iliyopita, watu 151 walipotea lakini 141 walipatikana kutokana na jitihada za Jeshi la Polisi. Hatuwezi kukubali hali hiyo iendelee na ni muhimu kuacha kunyoosheana vidole, bali tushirikiane kuimarisha usalama.”

Alihitimisha kwa kusema kuwa CCM imekasirishwa sana na tukio la mauaji ya Ali Kibao, na kwamba chama hicho kitaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wahusika wanakamatwa na sheria inachukua mkondo wake.

“Wakati tunasubiri hatua stahiki, tunasisitiza kuwa demokrasia lazima iendelee kushamiri. CCM inaamini katika mazungumzo, na tuna wajibu wa kushirikiana na kila mmoja kujenga taifa letu. Hatuna nchi nyingine,” alisisitiza Dk. Nchimbi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles