Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Asasi za kiraia nchini, kupitia Shirika la The Foundation for Civil Society (FCS), zimeiomba Serikali kuhakikisha makundi maalum, hususan watu wenye ulemavu, wanapatiwa miundombinu ya kidigitali ili waweze kushiriki kikamilifu katika michakato ya maendeleo na kujijenga kiuchumi.
Ombi hilo lilitolewa na Meneja Programu wa FCS, Nasim Losai, katika mkutano wa kitaifa wa watu wenye ulemavu, madiwani, na wadau uliofanyika Agosti 12, 2024, jijini Dar es Salaam. Losai alisema kuwa mkutano huo ulilenga kuimarisha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku ukizingatia matumizi ya takwimu za sensa katika kuboresha mipango ya halmashauri na ngazi za kata.
Aliongeza kuwa, ingawa Serikali imekuwa sikivu katika kusaidia makundi maalum, bado kuna haja ya kuendelea kuboresha juhudi hizi, hasa kwa kuhakikisha upatikanaji wa fursa za kiuchumi kupitia miundombinu bora. FCS, kwa zaidi ya miaka 20, imekuwa ikisaidia serikali katika shughuli za kijamii na kutetea haki za watu wenye ulemavu.
Mshauri mtaalam wa masuala ya watu wenye ulemavu nchini, Peter Charles, alibainisha kuwa mkutano huo ulihudhuriwa na watu wenye ulemavu zaidi ya 600 pamoja na madiwani 60 wa viti maalum kutoka Jiji la Dar es Salaam. Mkutano huo ulilenga kuwajengea uelewa watu wenye ulemavu kuhusu fursa za kiuchumi na changamoto zinazowakabili.
Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania, Hamadi Abdallah Komboza, alionyesha wasiwasi kuhusu upatikanaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu na kutoa wito kwa Kamishna wa Kazi kufanya ukaguzi kwenye mashirika na taasisi zinazopaswa kuajiri watu wenye ulemavu.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania, Jonas Lubalo, alishukuru taasisi ya Ikupa Trust Fund kwa mchango wake katika kusaidia watu wenye ulemavu nchini.