25 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

DC Mtwara atembelea Visima vya Gesi Asilia Nanguruwe

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital Mkuu wa Wilaya ya Mtwara,  Mwanahamisi Munkunda, amefanya ziara ya kutembelea visima vya gesi asilia katika kata ya Nanguruwe ambapo alitembelea kisima cha Ntorya-1 na Ntorya-2 ili kujionea maendeleo ya visima hivyo.

Meneja Mradi, Patrick Kabwe, alieleza kuwa licha ya maendeleo yaliyofanyika katika visima hivyo viwili, TPDC na kampuni ya ARA wanakusudia kuchimba kisima cha tatu, Chikumbi-1, ili kuongeza uzalishaji wa gesi asilia.

Mkuu wa Wilaya akiwa katika ziara kisma cha Ntorya-2 , Kata ya Nanguruwe.

“Sasa hivi tunakusudia kuanza uzalishaji wa gesi asilia kwa awamu. Awamu ya kwanza ya uzalishaji tunategemea kuanza mwezi Aprili, 2025, pamoja na hayo kutakuwa na uchorongaji wa kisima cha Chikumbi-1 katika kijiji cha Namayhakata. Visima vyote vitatu vikiwa kwenye uzalishaji vitazalisha hadi futi za ujazo milioni 60 kwa siku,” alisema Kabwe.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya alipongeza uongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuwa thabiti kwenye shughuli za utafutaji na uendelezaji wa nishati ya gesi asilia pamoja na kuwa mfano kwenye utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) mkoani Mtwara.

“Nawapongeza sana TPDC kwa kuendelea kuwekeza kwenye miradi ya gesi mkoani Mtwara. Kwa kwetu sisi, ni fursa kwani wananchi wanapata ajira, kuongezeka kwa pato la halmashauri kupitia mrabaha, pamoja na uboreshwaji wa huduma za kijamii kupitia CSR. Mfano mzuri ni ujenzi wa kituo cha afya cha Msimbati,” alisema Mkuu wa Wilaya.

Wananchi wa Nanguruwe wakifuatilia mkutano.

Ziara hiyo iliambatana na maafisa kutoka TPDC, ARA Petroleum, APY-KEGS Energy pamoja na Kamanda wa Polisi wa Wilaya. Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya alifanya kikao na wananchi wa Kata ya Nanguruwe kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wao kwenye mradi. Kikao hicho kilihudhuriwa na maafisa wa TPDC, ARA Petroleum, kampuni ya APY-KEGS Energy, pamoja na viongozi kutoka ngazi ya wilaya.

“Nitoe rai kwa wananchi wa Kata ya Nanguruwe kuwapokea wawekezaji pamoja na kutoa ushirikiano utakao hitajika,” alisema Mkuu wa Wilaya. Vilevile, Mwanahamisi alitoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha na kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwenye sekta ya gesi asilia mkoani Mtwara, hali inayoinua chachu ya maendeleo mkoani humo.

Mkuu wa Wilayaya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda akiongea na wananchi wa Nanguruwe.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles