Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
VIONGOZI wa vyama 13 vya siasa visivyokuwa na wabunge, wamepongeza hatua ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ya kuwateua na kuwajumuisha viongozi wa vyama visivyokuwa na wawakilishi kwenye Serikali yake, wakisema hatua hiyo imeimarisha demokrasia visiwani humo.
Jumamosi iliyopita Dk. Shein, aliwatangaza viongozi watatu kutoka vyama visivyokuwa na wabunge ambao ni Hamad Rashid Mohamed (ADC), Juma Khatib (Tadea) na Said Sudi (AFP) ambao wamejumuishwa katika Serikali yake.
Vyama vinavyounda umoja huo ni Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP), Sauti ya Umma (SAU), Union for Multiparty Democracy (UMD), Chama cha AFPÂ na Chama Cha Kijamii (CCK).
Wenyeviti wa vyama hivyo walitoa pongezi hizo jana walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari  na baadae kuzindua klabu yao.
Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa UMD, Kamana Masoud, alisema umefika wakati wa Rais Dk. John Magufuli naye kuiga mfano wa Rais Shein kuwateua viongozi kutoka vyama vingine ili washirikiane kuunda serikali.