25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

AngloGold Ashanti yamuahidi Samia kuwa kinara kuwezesha wanawake sekta ya madini

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

AngloGold Ashanti ambayo ni kampuni mama ya Geita Gold Mining Limited imemuahidi Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwa sehemu ya mabadiliko chanya ya ushiriki wa wanawake na usawa wa kijinsi mahala pa kazi, katika biashara na mahusiano ya wafanyakazi wao.

Makamu Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ubia na ushirika Afrika, Simon Shayo akihutubia katika maadhimisho ya Jukwaa la The Citizen Rising Women lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Hayo yamebainishwa wiki iliyopita Makamu Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ubia na ushirika Afrika, Simon Shayo akihutubia katika maadhimisho ya Jukwaa la The Citizen Rising Women lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Jukwaa hilo lililofanyika sambamba na kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake kimataifa lilichagizwa na kauli isemayo ’Wekeza kwa wanawake, ongeza kasi ya maendeleo.’

Aidha, Shayo alitoa rai kwa wadau na kampuni nyingine kuungana na Rais Samia aliyekuwa mgeni rasmi katika jukwaa hilo, katika kuitoa Tanzania mahala ilipo kuwa nchi ambayo itapigiwa mfano kwa maana kuwa suala la kukosa usawa wa kijinsia liwe la kihistoria.

“Tunakushukuru kwa kuendelea kuonesha njia, tunaishukuru sana Serikali kwa kuonesha kwa makusudi namna ambavyo wanawake wanaweza kushiriki kwenye nafasi za uongozi, hii tumeiona kwenye baraza la mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, taasisi na vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akikabidhi tuzo kwa Ofisa wa masuala ya sheria wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Elizabeth Karua kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo kudhamini Jukwaa la The Citizen Rising Women Forum lililofanya mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Alisema nchi ya Canada ambayo ndio moja ya vinara katika uchimbaji madini, ina asilimia 16 ya wanawake katika sekta ya madini hivyo, Tanzania imepiga hatua kupitia majukwaa hayo pamoja na juhudi wanazofanya za ushiriki zaidi wa wanawake katika sekta hii.

“Kampuni ya AngloGold Ashanti Mwenyekiti wa bodi ‘Group chair’ ni mwanamke, lakini viongozi watatu kati ya viongozi wakuu saba ni wanamke tena nyadhifa za muhimu kama chief financial officer, chief legal officer na chief people officer.

Alisema GGML pia haipo nyuma katika ushiriki wa wanawake kwenye uchimbaji kwani ni asilimia 13.

“Tunajikongoja lakini tupo karibu sana nchi ambazo zimepiga hatua kwenye uchimbaji. Tunayo malengo ya kuhakikisha kuna ushiriki wa wanawake ambao si kwenye nafasi za usaidizi bali hata ambazo wanaume wanashiriki.

“Tumehakikisha tunaleta wanafunzi kwenye uanagenzi na walau kukaa nao mwaka mmoja na tunahakikisha asilimia 50 ni wanawake, pia kwenye sera ya ajira tunapofanya upembuzi wa walioomba kazi lazima asilimia 50 iwe wanawake na wanapofungamana tunamchukua mwanamke,” alisema.

Alisema licha ya kwamba katika miaka mitatu -minne hapakuwa na nafasi za wanawake kwenye uongozi na sasa kupitia program ya Female Future Tanzania inayoendeshwa na Chama cha Waajiri Tanzaniza (ATE), wamefanikiwa kuwa wanawake wawili kwenye nafasi za menejimenti.

Pia alisema GGML imeanzisha kampeni mbili kubwa moja ni kampeni inayosema don’t cross the line pamoja na kampeni ya kupaza sauti zonazolenga kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia mahala pa kazi na wanaopatikana na hatia wanaondolewa kazini mara moja.

Akizungumzia maadhimisho  hayo ya siku ya wanawake duniani, Rais Samia alitoa wito kwa wanawake kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka kesho.

“Napenda kuhamasisha wanawake wenzangu kushiriki katika chaguzi hizi kwani wakifanikiwa kushinda katika nafasi zao patakuwa mojawapo ya jukwaa la kuzungumza na kutatua changamoto zinazowakabili wanawake,” alisema.

Alisema licha ya serikali yake kujitahidi kufikia usawa wa asilimia 50/50, malengo hayo hayawezi kufikiwa kirahisi bila kuwepo na malengo ambayo yanaenda sambamba na muamko kutoka ndani ya jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles