25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

JK, Ukawa wamtia Sitta kitanzani

Mtanzania 10092014NA RACHEL MRISHO, DODOMA

UAMUZI uliofikiwa na viongozi wa vyama vya siasa na Rais Jakaya Kikwete umemweka katika wakati mgumu Mwenyeki wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kuahirisha au la vikao vya Bunge hilo.

Hii inafuatia Rais Kikwete na viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kukubaliana kusitisha Bunge la Katiba Oktoba 4 tofauti na ratiba ya Sitta ambayo inaonyesha vikao vitaendelea hadi Oktoba 31 atakapomkabidhi rais katiba iliyopendekezwa.

Vilevile kwa tafsiri ya uamuzi huo, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watakuwa wameibuka kidedea kwani tangu mwanzo walikuwa wanataka Bunge hilo liahirishwe hadi maridhiano yapatikane.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, alisema katika makubaliano ya kikao chao na rais kilichofanyika juzi Ikulu ndogo mjini hapa, walikubaliana kwa pamoja kuwa Bunge la Katiba liendelee hadi Oktoba 4.

Kwa mujibu wa ratiba iliyokuwa imetolewa mara baada ya awamu ya pili ya Bunge la Katiba kuanza Oktoba 10 hadi 21, ndiyo wajumbe wa Bunge hilo walitarajiwa kuanza kupiga kura ili kupitisha sura mbalimbali za rasimu hiyo na kupata Katiba inayopendekezwa.

Alisema kuwa baada ya Bunge hilo kusitishwa, mabadiliko madogo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977  yatafanyika.

Alisema kuwa katika marekebisho hayo, sheria ya uchaguzi itafanyiwa marekebisho ili kuwezesha nchi kufanya uchaguzi ulio huru na wa haki.

“Pamoja na kazi ya msingi inayofanywa na Bunge Maalumu la Katiba, inaonekana kuwa mchakato huo unaoendelea sasa hauwezi kutupa Katiba itakayotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, muda hautatosha kukamilisha mchakato na kufanya mabadiliko yatakayohitajika,” alisema Cheyo.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya Katiba, mwisho wa mchakato huo ni kura ya maoni iliyotarajiwa kufanyika Aprili 2015.

“Kama itabidi kura irudiwe kwa mujibu wa sheria italazimika kura ya maoni ifanyike Juni au Julai 2015, muda ambao Bunge la Jamhuri ya Muungano linatakiwa livunjwe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015,” alisema mwenyekiti huyo.

Alisema hatua ya kura ya maoni haitafanyika tena kwa sababu itaingiliana na uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, alisema ili Katiba mpya ipatikane na kutumika katika uchaguzi mkuu ujao, ni lazima uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya mwaka 2015, jambo ambalo alidai kuwa haliungwi mkono na TCD.

Cheyo alieleza kuwa mchakato wa kupata Katiba mpya ambao utasitishwa Oktoba 4, utaendelea baada ya uchaguzi mkuu mwakani.

Alisema kwa vile uchaguzi mkuu utafanyika kwa kutumia Katiba ya sasa, wamekubaliana kwa pamoja mambo ya msingi yafanyiwe mabadiliko ndani ya Katiba hiyo.

Mambo yatakayorekebishwa kwenye Katiba ya 1977

Mambo yatakayorekebishwa kwenye Katiba ya 1977 ni pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi na mshindi wa uchaguzi wa nafasi ya rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50.

Mambo mengine ya kuingizwa kwenye Katiba ni pamoja na  matokeo ya urais kupingwa mahakamani na  kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi.

Alisema kuwa vyama vya siasa ambavyo vinapenda kupendekeza mambo mengine ya kufanyiwa marekebisho katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano 1977, vimeombwa kufanya hivyo mapema kwa kuwa muda uliobaki ni mdogo.

“TCD kupitia vikao vyake itakaa kujadili mapendekezo hayo na kuyapeleka serikalini kwa hatua nyingine,” alisema Cheyo.

Mkakati wa Sitta

Mara tu baada ya awamu ya pili ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza, marekebisho ya kanuni yalifanyika ambapo muda wa Bunge hilo uliongezwa.

Kutokana na marekebisho hayo, hatua ya kupiga kura ili kupitisha ibara mbalimbali za Rasimu ya Katiba, ilitarajiwa kuanza Oktoba 10 hadi 21.

Baada ya siku moja ya kufanya marekebisho kanuni, kamati za Bunge hilo zilikaa kwa siku 17 kupitia sura 15 za Rasimu hiyo zilizokuwa zimebaki baada ya awamu ya kwanza ya Bunge hilo kupitia sura ya kwanza na ya sita.

Ratiba hiyo ilionyesha kuwa kazi ya kamati kupitia sura hizo ilitakiwa kukamilika Agosti 27, mwaka huu.

Kati ya Agosti 28 hadi Septemba mosi, kamati hizo zilitakiwa kukamilisha kazi ya kuandaa taarifa ya sura zote walizozijadili.

Kwa mujibu wa ratiba, Septemba 2 hadi 8 kamati hizo ndipo zilifanya kazi ya kuwasilisha taarifa zao ndani ya Bunge Maalumu ili zianze kujadiliwa.

Baada ya kazi hiyo kukamilika juzi, jana wajumbe wa Bunge hilo walianza mjadala wa kuchagia kwenye sura zilizowasilishwa, kazi iliyotarajiwa kufanyika kwa siku 15 hadi kufikia Septemba 29.

Majadiliano yakimalizika Kamati ya Uandishi itaanza kazi ya kuandika upya ibara za sura zote za Rasimu ya Katiba kazi itakayofanyika kwa muda wa siku tano, Septemba 30 hadi Oktoba 6.

Oktoba 9, Kamati ya Uandishi ilitarajiwa kuwasilisha taarifa yake katika Bunge Maalumu kuhusu rasimu hiyo ili iweze kupigiwa kura na kazi hiyo ya kupiga kura ndipo itaanza Oktoba 10.

Kati ya Oktoba 22 hadi 28, wajumbe wa Bunge hilo walitarajiwa kupitisha masharti ya mpito.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Oktoba 29 na 30 ni siku ambazo Katibu wa Bunge atakamilisha Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kuwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar.

Ratiba hiyo inaeleza kwamba Oktoba 31 ni siku ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Sitta kuwasilisha Katiba inayopendekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

4 COMMENTS

  1. Sasa hitimisho la kupatikana kwa Katiba Mpya chini ya utawala wa Kikwete limefungwa. Limefungwa kutokana na Rais Kikwete kushindwa kusimamia kwa umakini ahadi ya katiba mpya wa Watanzania. Nyaraka mbalimbali zinaonesha kuwa Bunge hili la katiba mpaka sasa limefanikiwa kutumia shilingi bilioni 200. Pesa hizi ni nyingi sana kiasi kwamba kama CCM hawakuwa na mpango wa kupata katiba mpya pesa hizi zingesaidia kununulia madawati ili kuwaepushia watoto wa wakulima kuendelea kuota vibiyongo kwa kukaa chini. Mungu Ibariki Tanzania.

  2. Kwanza napenda kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais Kikwete kwa maono ya Mungu aliyompa na kuafiki kukaa kikao na waheshimiwa waliokuwa na upingamizi jinsi muundo wa Bunge la katika unavyofanyika. Rais ni ngazi ya mwisho katika nchi katika maamuzi yoyote. Ni mambo Mungu ameonyesha kwake kutokana na udhaifu uliopo. Makubaliano yao tunashukuru watanzania wote kwani yamekwenda vizuri na mariadhiano yamekubalika na ndio watanzania wengi tulikuwa tunaliomba hilo kila kukicha ili kusitokee mintafaruku kama yaliyojitokeza kwa ndugu zetu wengine katika nchi zao. Bunge linaloendelea sidhani lina manufaa yoyote zaidi hata kama lingekaa kutimiza sheria iliyokukuwa imepitishwa kwa muda huo wa siku 60. ni majadialiano ambayo yapo kinyume na makubaliano ya rasimu ya mheshimiwa Warioba kufuatana na maoni ya wananchi waliokwisha yatoa. Ningemwomba Mheshimiwa Spika wa Bunge letu kutumia democrasia ambayo itaweza ikasitisha mwendelezo wa kuichambua rasimu hiyo ya katiba na katika hilo kuungana na maridhiano ya Mheshimiwa Rais na TCD ili majadiliano yaweze kuja kujadiliwa kwa makubaliano ambayo kila upande utaridhika nayo na kuunda katiba inayokubalika na watanzania wote. hakuna raia yoyote wa Tanzania anayependa vurugu. Baba yetu Marehemu Nyerere alituacha katika hali ya amani ya upendo ya kukosoana kwa haki na amani na alituacha bia kuona vurugu ya mapigano. Vizazi vyetu tumekuwa na maingiliano ya kupendana naweza kupenda kutoka katika ncha yoyote ya Tanzania. Je? vurugu ikitokea kama leo hii je si tutauana ndugu kwa ndugu? Tumshukuru Mungu na kuendelea kuiombea serikali yetu na watendaji wote Mungu aweze kuwapa maono ya upendo katika kufanikisha kazi hii. MUNGU IBARIKI TANZANIA.

  3. Ni ukweli usiofichika kwamba Rais tulienae ni mtu mwenye hekima na busara za hali ya juu licha ya kuchafuliwa heshima yake na wasaka tonge.Wasaka tonge waliweza kujiongezea siku kinyemela za kukaa kwenye ulaji wakijua kua katiba wanayoitunga haina maslahi kwa wananchi.Wasaka tonge walifanya kwa makusudi kutokuweka kipengele cha kuvunjwa kwa bunge na Rais endapo mambo yangekwenda ndivyo sivyo.Wasaka tonge kwa makusudi waliamua kukipaka matope chama cha mapinduzi wakijifanya wanakipenda.Hatima ya yote waliokuwa wakishauriwa kutokuendelea na bunge wakayakataa yamefikia wapi.Watu makini na waaminifu akina Mchemba,waliyaona haya na walipendekeza kutokuendelea na Bunge.Lakini wapi!Dikteta anaeinyemelea nchi kwa udi na uvumba alikua hakubaliani na lolote wala chochote.Mungu awabariki Wastanzania na Tunampongeza Rais na wadau wenzake kwa maamuzi yao ya busara.

  4. Mwenyekiti wa Bunge la Katiba angekuwa na busara kidogo angasitisha vikao vinavyoendelea kwa sasa. Yote haya aliyawma Mhe Mwigulu Nchemba na hii inaonyesha aliyaona haya yote kuwa fedha za walipakodi zinapotea bure, next time yafaa Mhe Nchemba awe ndiyo mwenyikiti mpya wa bunge la katiba baada ya Rais mpya kupatikana 2015!!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles