25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Simba akiri ngono kukithiri shule za msingi

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba

SHABANI MATUTU NA AZIZA MASOUD

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, amesema utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), kuhusu wanafunzi wa shule za msingi kujihusisha na ngono una ukweli.

Simba ameyasema hayo baada ya gazeti hili kutoa taarifa kuhusu matokeo ya utafiti uliofanywa na MUHAS kupitia mradi wa PREPARE yaliyotolewa wiki iliyopita ili kubaini vijana wanaofanya ngono katika umri mdogo.

Akizungumza na MTANZANIA, Waziri Simba ameumwagia sifa utafiti huo na kusema kuwa ni mzuri na alitoa wito kwa wazazi na walimu kutoa elimu ya uzazi majumbani na shuleni kwa watoto.

Alisema kuwa sababu kubwa ya wanafunzi hao kujiingiza katika vitendo hivyo imechangiwa na kutoijua elimu ya uzazi na kutoelekezwa athari zake.

“Nimekuwa nikiwasihi wazazi mara kadhaa waanze kuwafundisha vijana wao madhara yanayotokana na kufanya mapenzi katika umri mdogo, wenzetu huko nje wamekuwa wakiwaeleza vijana wao kwamba mtoto anakaa tumboni, lakini hapa kwetu tunaficha, tukidhani tukisema tutakuwa tunawafundisha,” alisema.

Waziri Simba aliongeza kuwa dhana hiyo ndiyo imekuwa sababu kubwa ya vijana hao kujikuta wakijaribu kufanya wenyewe ili kujifunza.

“Nchi zilizoendelea wazazi wamekuwa wakiwaeleza watoto wao madhara ya kubakwa na njia ambazo wabakaji wamekuwa wakitumia, lakini kwetu ndiyo tunawafundisha watoto wetu kuzungumza na watu wasiowajua tukifikiri ndiyo heshima bila ya kujua si wote wenye nia njema kwani wengine ni wabakaji,” alisema.

Alitoa wito kwa wazazi na walimu kuwaeleza madhara yatakayowapata watoto wao wa kiume pindi watakapojihusisha na kufanya vitendo vya ngono ya jinsia moja.

Katika utafiti wa MUHAS, imebainika kuwa asilimia 10 ya vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 14 ambao ni wanafunzi wa darasa la tano na sita wameshawahi kufanya ngono, ambapo kwa asilimia kubwa wamekuwa wakifanya kinyume na maumbile, wengine wakifanya kwa njia ya kawaida na mdomoni.

Utafiti huo wa miaka minne ambao ni mradi wa PREPARE, ulishirikisha Chuo Kikuu cha Makerere cha Uganda, Cape Town na Limpopo vya Afrika Kusini, Bergen na Oslo vya Norway, Maastricht cha Uholanzi na Sussex cha Uingereza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles