Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua Mkutano wa kwanza wa kitaifa wa Dira ya Maendeleo ya Taifa utakaofanyika Disemba 9, 2023 katika Kituo chaMikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 1, 2023 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema jumla ya wadau 971 wamealikwa kushiriki mkutano huo na utahudhuriwa na makundi maalum na viongozi mbalimbali nchini.
Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuzindua, kupokea na kujadili taarifa ya kitafiti ya tathmini ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa 2025.
“Dk. Samia atazindua rasmi timu kuu ya kitaalam ya dira na kamati ya usimamizi wa dira pamoja na nyenzo za kidigitali zitakazotumika katika kukusanya maoni ya wadau, “amesema Profesa Mkumbo.
Amesema taarifa ya kitafiti ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na mengine na imeainisha mafanikio yanayopatikana na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa dira hiyo.
Amesema dira hiyo ilianza kutelezwa mwaka 2000 na inafikia mwisho wake mwaka 2025, pamoja na mafanikio mengine taarifa ya tathimini inaonesha pato la mtanzania limeongezeka kutoka dola za Kimarekani 399.5 mwaka 2000 hadi kufikia dola 1200.
“Tanzania imefikia asilimia 124 ya kujitosheleza kwa chakula ilikulinganishwa na lengo la kufikia asilimia 140 ifikapo mwaka 2025 na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kutoka vifo 760 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2000 hadi kufikia 104 mwaka 2022 ikiwa tumevuka lengo la kufikia vifo 265 ifikapo mwaka 2025 ni matokeo kamili ya tathimini hii,”amesema.
Ameongeza kuwa wameanza mchakato wa kuandaa Dira mapya ya 2050, huku akiwaomba wananchi kufuatilia mchakato huo na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kuhusu Tanzania waitakayo katika miaka ijayo.
Aidha amesema kwa kuwa mkutano huo unafanyika siku ya uhuru Rais Samia atatumia siku hiyo kutoa ujumbe maalumu katika maadhimisho miaka 62 ya uhuru.