Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Mashindano ya vijana yanayoitwa ‘ Just Fit Inter Schools Games’, yanatarajia kufanyika Disemba 9-10, 2023 yakihusisha michezo mitano tofauti itakayofanyika kwenye viwanja vya Gymkhana, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 20, 2023 leo Dar es Salaam, Meneja masoko wa Just Fit , Jabir Jabir amesema michezo itakayokuwepo katika mashindano hayo ni kikapu, soka, chess, kuogelea na tenisi, lengo likiwa ni kukuza vipaji na kuwajengea vijana tabia ya kupenda michezo.
Amesema mashindano hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza lakini yatakuwa yakifanyika kila mwaka kuanzia sasa ili kuibua vipaji ambayo baadaye vitakuwa juu kama kina Hashim Thabit, Mbwana Samatta, Fei Toto, John Bocco na wengine wanaofanya vizuri kitaifa na Kimataifa.
‘Lengo la kuanzisha ‘Just Fit Inter Schools Games’ ni kujenga tabia ya kupenda michezo kwa vijana/watoto. Ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada zake za kukuza vipaji vya michezo kuanzia rika la chini, yaani kwa watoto au vijana wadogo.
Amewaomba wadhamini wengine wataka kushirikiana nao kujitokeza ili kuunga mkono jitihada hizo kwani ni jambo ambalo linakwenda kutengeneza wanamichezo wa baadaye.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi wa Justfit Foundation, Begam Sykes, amesema dhumuni lao ni kurudisha kile walichokipata kwa jamii ambapo asilimia 10 ya kile kitakachopatikana kupitia mashindano hayo watatumia kukarabati baadhi ya viwanja.