26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Ufinyu wa bajeti unavyokwamisha kilimo Buchosa

*Pikipiki za Serikali zageuka kero badala ya msaada

*Maafisa waishi kwakutegemea wakulima

Na Clara Matimo, Aliyekuwa Buchosa

Mwaka 2022 Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuboresha na kuinua sekta ya kilimo ilitoa Pikipiki 7,000 kwa Maafisa Ugani katika halmashauri 140 kwenye mikoa 25 nchini ili kuwawezesha kufanya kazi vizuri na kuwahudumia wakulima ili iweze kuwa na tija kubwa kwa Taifa.

Sambamba na hilo, kila mwaka Serikali imekuwa ikitoa mwongozo kwa halmashauri zote nchini kutenga asilimia 20 ya mapato ya ndani ili kuboresha sekta ya kilimo na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo katika eneo husika.

Mwandishi wa makala haya (katikati) akiwa na Afisa Kilimo Kata ya Bukokwa, Jackson Masatu (wa kwanza kulia) pamoja na mkulima Amos Bush (mwenye kofia) alipomtembelea shambani kwake hivi karibuni

Januari 17, 2023 wakati Serikali akigawa pikipiki hizo, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango alitoa maagizo kwa Wakurugenzi wa halmashauri, miji na manispaa kutenga fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za maafisa ugani katika maeneo yao huku akiwataka maafisa ugani hao kuhakikisha wanazitumia vyema pikipiki hizo ili kuwasaidia wafugaji kufanya ufugaji wenye tija.

Hata hivyo, licha ya jitihada hizo kasi ya utekelezaji wa mwongozo huo imekuwa yakusuasua. Baadhi ya sababu zinazotajwa na wadau wa kilimo ni ufinyu wa bajeti na kukosekana kwa sheria ya muongozo huo.

Katika kufahamu kwa undani juu ya utekelezaji huo na changamoto zake, Mtanzania Digital imefanya mahojiano maalum na wakulima ndani ya Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza na baadhi ya watendaji wa sekta ya kilimo ambao wanakiri kuwapo kwa changamoto huku kupendekeza baadhi ya njia wanazoamini kuwa zitasaidia kuleta ahueni kwa ustawi wa sekta ya kilimo nchini.

Wakulima wanasemaje

Akizungumza na Mtanzania Digital Mkulima, Patrick Hadohado ambaye ni mkazi wa Kata ya Nyehunge, anasema imekuwa vigumu kutekelezwa kwakuwa haujatungiwa sheria ya kuwabana wakurugenzi wa halmashauri kuutekeleza kwa vitendo na kwamba kama mwongozo huo ukitekelezwa utawasaidia wakulima kutatua changamoto zilizopo lakini.

Aidha, anaiomba serikali kuongeza wataalamu wa ugani kwani waliopo hawakidhi mahitaji ya wakulima.

“Kwa mfano hapa Nyehunge kata yetu pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wakulima lakini ina mtaalamu mmoja tu wa kilimo ambaye huwa ananitembelea na kunipa ushauri. Tunashukuru imetoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima na mimi ni mnufaika na tayari msimu huu nimepata mbolea na nimeitumia kwenye shamba langu kuoteshea na baadaye nitaweka mbolea ya kukuzia mazao,” anasema Hadohado.

Afisa Kilimo kata ya Nyehunge Halmashauri ya Buchosa, Abel Sato akitoa elimu kwa mkulima wa Kata hiyo.

Kauli hiyo ya upungufu wa maafisa ugani inaungwa mkono na mkulima wa mwingine ndani ya kata hiyo, Elizabeth James ambaye ameiomba serikali kutunga sheria itakayowabana wakurugenzi wa halmashauri kutenga bajeti na kuwanufaisha wakulima watakaolima kwa tija baada ya changamoto zilizopo kutatuliwa ikiwamo upungufu wa wataalam wa kilimo.

Wako tayari kulima

Wakati Kata ya Nyehunge wakilia na upungufu wa maafisa ugani, upande wake, Twindalwesile Richard kutoka kata ya Bukokwa anasema wakulima hususan wadogo wana changamoto nyingi ikiwamo miundombinu kwenye kilimo cha umwagiliaji kwani wanalima kwa kutegemea mvua ambazo hazina uhakika lakini halmashauri ikitenga fedha kwa ajili ya kukuza sekta hiyo watalima kwa tija na kunufaika zaidi.

“Naishauri serikali ituangalie wakulima ili tuwe na kilimo cha uhakika kwa kutumia teknolojia za umwagiliaji maana tunavyolima kwa kutegemea mvua kuna wakati inachelewa kunyesha au kuwa hafifu hivyo tunakosa mazao tuliyotarajia hasa yale ya mapema,” anasema Richard.

Mafuta yakwamisha wataalam

Abel Sato ni Afisa Kilimo Kata ya Nyehunge ambaye licha ya kata hiyo kuwa na wakulima 19,650 lakini ana uwezo wakuwafikia wakulima 200 tu.

Hii ni sawa nakusema kwamba wakulima 19,450 wanakosa huduma hiyo ya maarifa kutoka kwa mtaalam huyu aliyeaminiwa na serikali kwa ajili ya kunyanyua kilimo kanda hii ya Buchosa.

Sato anasema kuwa changamoto kubwa imekuwa ni kukosa mafuta ya kuweka kwenye pikipiki kwa ajili ya kutembelea vijiji vyote, sambamba na hilo wanakosa pia fedha za kufanyia pikipiki hizo matengenezo pindi zinapoharibika na kulazimika kutumia fedha zao binafsi jambo ambalo ni gumu kulimudu kwa muda mrefu.

“Lengo langu kwa siku nikuwafikia wakulima 10, lakini nawafikia watatu au wanne kwa sababu si kwamba nitawakuta wakulima wengi shambani kwa wakati mmoja na wakati mwingine nachelewa kwa mkulima mmoja kutokana na changamoto nitakayomkuta nayo,” anasema Sato na kuongeza:

“Hata hivyo kuna nafuu kidogo kwa sasa kwani nawahudumia wengi kutokana na mfumo wa M-Kilimo ambao serikali imetuletea pia baadhi wananipigia simu na kwa wale wanaoelewa umuhimu wa nafasi yangu kama afisa ugani anaweza akakupa lita moja ya mafuta au akakufuata kwa gharama zake ili kushughulikia changamoto zake kama tatizo halihitaji nifike shambani kwake namuelekeza mkulima namna ya kulitatua kwa njia ya simu,” anasema mtaalamu huyo.

Naye, Afisa Kilimo Kata ya Bukokwa, Jackson Masatu anasema katika eneo lake kuna wakulima takribani 8,000 lakini ana uwezo wa kuwafikia na kutoa msaada kwa wakulima 200 kutokana na changamoto ya gharama za mafuta ya pikipiki huku akiiomba serikali kupitia halmashauri kuweka fungu ili waweze kuwafikia wakulima wengi na kukidhi mahitaji ya wakulima wanaohitaji utaalam kutoka kwao.

“Asilimia 20 ya bajeti ambayo serikali imeagiza kila halmashauri kutenga kwa ajili ya sekta ya kilimo nadhani huwa inaishia kutamkwa tu kwenye vyombo vya habari na makaratasi maana kama ingekuwa inatekelezwa kikamilifu nadhani hata kuweka ruzuku kwenye mbegu, mbolea na wataalam kupata mafuta na matengenezo ya pikipiki yangefanyika.

“Hivyo, serikali itunge sheria na iweze kuisimamia kikamilifu si tu kutunga sheria na kuiweka kwenye makabati, itunge sheria na iisimamie ili ilete ufanisi kwenye sekta hii,” anasema Masatu.

Afisa Kilimo Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza, Nestory Mjojo akifafanua jambo kwa mwandishi wa makala haya (hayupo pichani).

Hata hivyo, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Buchosa yenye kata 21 zikiwa na jumla ya wakulima 160,000, Nestory Mjojo anasema hatua ya serikali kugawa pikipiki kwa maafisa ugani haitoshi kwani vyombo hivyo vya usafiri vinahitaji mafuta na matengenezo kila siku ili kumrahisishia afisa huyo kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi na kufikia malengo ya serikali kukuza sekta hiyo.

“Ikitungwa sheria itasaidia kushughulikia masuala ya huduma za ugani na pikipiki zitahudumiwa na serikali hivyo hazitachakaa mapema, zitakuwa na mafuta pia itaingia katika pembejeo za kilimo na kupunguza gharama za kusafirisha mbolea,” anasema Mjojo.

Hali ilivyo Buchosa

Katika Mwaka wa Fedha 2023/24 Halmashauri ya Buchosa imetenga Sh 73,000,000 kwenye sekta ya kilimo sawa na asilimia mbili ya bajeti yake ambayo ni Sh 3,830,775,000, kiwango ambacho ni cha chini ukilinganisha na miaka minne iliyopita.

Matharani, katika Mwaka wa Fedha 2022/23 bajeti ya halmashauri hiyo ilikuwa ni Sh 3,030,723,920 huku fungu lililotengwa kwa ajili ya sekta ya kilimo likiwa ni Sh 314,485,000 sawa na asilimia 10.

Mwaka 2021/22, halmashauri hiyo iliitengea sekta ya kilimo Sh 170,468,700 sawa na asilimia 5.2 ya bajeti yote Sh 3,220,456,920.

Vilevile, mwaka 2020/2021 Sh 170,000,000 zilitengwa kwa ajili ya sekta ya kilimo sawa na asilimia 5.2 kati ya Sh 3,226,571,000 za bajeti ya halmashauri hiyo.

Huku, mwaka 2019/2020 sekta ya kilimo ikitengewa Sh 174,000,000 sawa na asilimia 6.4 ya Sh 2,700,000,000 za bajeti ya halmashauri hiyo.

Nini kifanyike

Sato ambaye ni Afisa Kilimo Kata ya Nyehunge, anasema kutungwa kwa sheria itakayoweka mkazo na kuzibana halmashauri ndiyo mwarobaini wa matatizo mengi katika sekta hiyo kwani itasaidia pikipiki za maafisa ugani kutengenezwa, kuwekewa mafuta na kuwafikia wakulima wengi ambao watapata ushauri na utaalam, hivyo kufanya kilimo chenye tija.

“Ombi langu kwa serikali itunge sheria hapo tutapata mwarobaini wa changamoto zinazoikabili sekta yetu ya kilimo, pikipiki zetu tulizopewa zitatengenezwa, tutawekewa mafuta nasi tutawafikia wakulima wengi maana sasa inabidi ili nimfikie mkulima nitoe pesa yangu mfukoni niweke mafuta au mkulima ambaye ni muelewa anakuwezesha mafuta ili umfikie,” anashauri Sato.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Buchosa, Nestory Mjojo anasema kuna wakati wanahitaji taarifa za mwenendo wa kilimo kutoka maeneo mbalimbali lakini wanashindwa kuzipata kwa wakati kwa sababu maofisa kilimo na ugani wanadai hawana vifaa na vitendea kazi kuwasaidia kukusanya taarifa hizo kutokana na ufinyu wa bajeti.

“Kwa mfano kwa sasa kuingiza data kwenye mifumo unahitaji fedha sasa kama mwongozo usipotekelezeka unajikuta unatumia pesa yako ya mfukoni jambo ambalo ni gumu sana kwa kweli, unahitaji kupakia na kupakua nyaraka mbalimbali kwa kutumia intaneti sasa unaweza ukajikuta huwezi kufanya kazi kwahiyo bila huu mwongozo kutekelezwa lazima sekta ya kilimo iyumbe.

“Na sekta hii ndiyo inapaswa ichukuliwe katika uzito wa hali ya juu sana maana mabwana shamba au sisi tukishindwa tu kuwajibika vizuri halmashauri inaingia kwenye njaa na ikiishaingia kwenye njaa maana yake hata mipango mingine itasimama maana huwezi kwenda kuhamasisha watu shughuli  za maendeleo wakati wana njaa. Mimi nashauri itungwe sheria kama iliyotungwa ya kuwainua wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kutenga asilimia 10 kwa ajili ya kuwakopesha,” anasema Mjojo na kuongeza:

“Hata Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anapokuja kukagua anakagua kama pesa hiyo imetengwa na imewafikia walengwa lakini huu mwongozo wetu hauwezi kukaguliwa kwa sababu si sheria na hakuna mtu anayeweza kuhoji. Na sisi maafisa kilimo tunapokutana kwenye vikao vyetu tumekuwa tukisisitiza sana kwamba iwekwe sheria ili kutekeleza mwongozo huo,” anasisitiza Mjojo.

Mdau wa kilimo kutoka Shirika liliso la Serikali linalojishughulisha na uchumi wa nyumbani (TAHEA), Mussa Masongo anashauri serikali kuja na mpango wa taifa katika sekta ya kilimo unaozingatia mahitaji ya kila eneo na kuwepo na dira ya taifa ya maendeleo na mikakati madhubuti ili kutokomeza umaskini ifikapo mwaka 2030.

“Lazima tujue rasilimali zipi zinapatikana wapi na zitawafikiaje wakulima na serikali inapopanga bajeti yake iangalie vipaumbele vya kila wilaya na visibadilishwe maana vipaumbele vya halmashauri vimekuwa vikibadilishwa kutokana na vipaumbele vya taifa mfano wakulima wana shida ya wataalam wa kilimo lakini sisi kama taifa tunawapelekea mbolea kwahiyo lazima mkulima abaki njia panda, ni lazima tupime na kuwajengea uwezo maafisa wetu, bajeti itengwe kama serikali imeamua kuwekeza,” anashauri Masongo.

Sambamba na hayo, anasema: “Kama serikali itatunga sheria maelekezo hayo yatatekelezwa lakini maelekezo ya waraka bila kifungu hayawezi kutekelezeka kama walivyosema asilimia 10 kwa makundi maalum kwa kutunga sheria.

“Changamoto ni kwamba mabwana shamba wengi hawana mashamba ya mfano ambayo yangewasaidia wakulima kwenda kujifunza, kwanini mimi ambaye sina taaluma ya masula ya kilimo niwekeze fedha zangu katika kilimo wakati mwenye taaluma hiyo hajawekeza lazima tuwe na mashamba ya mfano labda afisa kilimo wa wilaya au kata ana shamba na wakulima wanaenda kujifunza kwake,” anasema.

Anasema yeye binafsi anaunga mkono ushauri uliotolewa na wadau wa sekta ya kilimo kuiomba serikali kutunga sheria itakayozibana halmashauri kutenga fedha hizo kwa ajili ya kuendeleza kilimo nchini.

Ikumbukwe kuwa pamoja na makala haya kuangazia halmashauri ya Buchosa lakini uhalisia wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya sekta ya kilimo unafanana kwa halmashauri nyingi hapa nchini.

Mkulima wa mahindi, Musa Bunela wa Kijiji cha Nyamadoke Kata ya Nyehunge halmashauri ya Buchosa wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza akiangalia mahindi yake ambayo yameshambuliwa na ugonjwa.

Mnyororo wa thamani wa kilimo unaanzia katika huduma, hivyo kama hakuna huduma ina maana maafisa kilimo hawawezi kuwajibika vizuri kwa wapokea huduma .

Kwa mfano ikiwa kata ina wakulima takribani 19,000 lakini wanaofikiwa na kupewa elimu ya kilimo bora  au namna ya kukabiliana na magonjwa kwenye mazao ni 200 tu ni wazi kuwa kuna safari ndefu kufikia lengo la kilimo kuchangia asilimia 10 ya pato la taifa ifikapo mwaka 2030.

Naamini serikali yetu sikivu inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri wake makini aliyemteua kwenye sekta hiyo nyeti na muhimu, Hussein Bashe, itafanyia kazi changamoto hiyo ya wadau katika sekta ya kilimo.

Hii ni pamoja na kutunga sheria ili asilimia 20 ya fedha iwe inatolewa kwa ajili ya kuboresha sekta ya kilimo kwani iwapo hilo litafanikiwa vijana wengi wanaoishi vijijini ambako kilimo kinafanywa kwa asilimia kubwa hawatakuwa na haja ya kukimbilia mijini kwa lengo la kutafuta maisha bali watajikita katika shughuli za kilimo kwa kuwa huduma za ugani zitaboreshwa pia watapata pembejeo bora na kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles