29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sababu, kinga ya harufu mbaya ya kinywa

kinywa 2Na Hamisa Maganga, Dar es Salaam

IDADI kubwa ya watu duniani huwa na harufu mbaya ya kinywa hasa baada ya kutoka kulala, kutokula na kunywa au kuzungumza kwa muda mrefu. Utafiti uliofanywa miaka kadhaa iliyopita na madaktari bingwa, ulibaini kuwa asilimia 25 ya watu duniani kote huwa na tatizo sugu la harufu mbaya ya kinywa.

Walibaini kuwa bakteria wanaotoa gesi kutoka kwenye ulimi na chini ya fizi ndio wanaochangia kwa kiasi kikubwa harufu ya uozo kinywani.
Aidha, wakati mwingine harufu mbaya hutoka katika matundu ya meno, ugonjwa wa fizi na mafindofindo (tonses) pindi yanaponasa mabaki ya chakula.
TDA yaadhimisha Siku ya Afya ya Kinywa

Machi 20 mwaka huu, Chama cha Madaktari wa Kinywa na Meno Tanzania (TDA), kiliadhimisha Siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani (WOHD).

Katika maadhimisho hayo, madaktari hao walibainisha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watoto walio chini ya miaka 14, wanakabiliwa na magonjwa ya kinywa na meno wakati asilimia 80 ya Watanzania wanakabiliwa na matatizo ya ugonjwa wa fizi.

Maadhimisho hayo yaliyobeba kaulimbiu ya ‘Afya Njema ya Kinywa, Afya Njema ya Mwili’, yaliyoanza Machi 13 hadi 20 mwaka huu, yalilenga kuhamasisha, kuelimisha na kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno kwa watu mbalimbali nchini.

Makamu wa Rais wa TDA, Dk. Ambege Mwakatobe, ambaye pia ni daktari bingwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anasema ugonjwa wa kinywa na meno hasa kutoboka kwa meno huwaathiri zaidi watoto.

Anasema kuwa watoto wanaathirika zaidi kwa sababu ya kupenda kula vyakula vya sukari ambavyo huathiri meno kwa asilimia kubwa.

Naye Rais wa TDA, Dk. Lorna Carneiro, anasema tafiti nyingi duniani zinaonyesha kuwa bado tatizo la kinywa na meno ni kubwa, hivyo watu wanapaswa kujikinga kwa kupatiwa elimu kuhusu afya ya kinywa.

 

kinywa 5Fastjet yafadhili safari ya TDA

Ili kuhakikisha kuwa TDA inawafikia watoto wenye ulemavu kwa lengo la kuchunguza na kuwapatia matibabu ya kinywa na meno kwa wale walioathirika, Shirika la Ndege la Fastjet Tanzania, lilidhamini chama hicho kwa kutoa tiketi tisa za ndege kutoka Dar es Salaam hadi mkoani Shinyanga ili kuwawezesha kutoa huduma ya afya na usafi wa kinywa katika  kituo hicho.

Mwenyekiti wa TDA aliyemaliza muda wake, Dk. Rachel Mhaville, anasema msaada huo ulikuwa unahitajika mno ili kuwezesha chama hicho kutoa huduma na tiba kwa watoto hao.

“Tunaishukuru kwa dhati Fastjet ambayo imetupatia tiketi zilizowezesha madaktari wetu  kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Shinyanga kutoa huduma ya afya ya kinywa kwa watoto zaidi ya 250… tunaichukulia Fastjet kama ‘malaika wetu mlinzi’,” anasema Dk. Mhaville.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Umma kutoka Fastjet, Lucy Mbogoro, anasema shirika hilo lina programu kubwa ya huduma za jamii ambazo lengo lake ni kusaidia shughuli zilizopo kwenye mtazamo wa elimu, afya/ustawi wa jamii na mazingira ili kuchangia kuboresha maisha ya watu wahitaji ndani ya jamii.

“Fastjet inaelewa changamoto zinazoikabili sekta ya afya katika  suala zima la kutoa huduma muhimu kwa jamii, ndiyo maana  tumetambua kuwa afya ni miongoni mwa vipaumbele vya msingi vinavyohitaji kuungwa mkono.

“Ni matumaini yetu kwamba mtakwenda mbali katika kuwasaidia watu walio na uhitaji, hususani wale ambao wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi ndani ya jamii,” anasema Mbogoro na kuongeza kuwa shirika hilo limejitoa kusaidia nyanja hizo ambazo zina manufaa.

Akizungumzia kuhusu afya ya kinywa, Dk. Mhaville anasema zaidi ya asilimia 90 ya idadi ya watu duniani wanakabiliwa na magonjwa ya kinywa katika maisha yao, lakini yaliyo mengi miongoni mwake  yanaweza kuepukwa kwa  kuongeza kiwango cha matibabu.

Anaitaka Serikali, wadau wa sekta ya afya na jamii kwa jumla  kuwaunga mkono ili waweze kuzuia maradhi ya kinywa, hatimaye kuhakikisha afya ya kinywa inakuwapo ndani ya jamii.

Anasema TDA imechagua kituo cha Buhangija kwa kuwa kinalea watoto waliokosa haki ya msingi ndani ya jamii, wakiwamo wenye albino ambao wanapata tabu kuzifikia huduma za afya za kutosha.

Mwaka jana Fastjet iliwasafirisha madaktari hao hadi kwenye kituo hicho ambapo watu zaidi ya 300 wakiwamo watoto, walimu na wafanyakazi wengine walinufaika kwa kupata huduma za afya ya kinywa.

 

Mkuu wa Kituo Buhangija anena

 

Mkuu wa kituo cha kulea watoto wenye ulemavu Buhangija, Peter Ajali, anasema watoto hao wanakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa zaidi ni walezi kutelekeza watoto wao kituoni hapo bila ya kwenda kuwasabahi.

Anasema kuwa hali hiyo inawafanya watoto wateseke kwa magonjwa mbalimbali yakiwamo ya kinywa na meno.

Naye mlezi wa watoto hao, Digna Mwacha, ambaye pia ni mlemavu wa ngozi, anasema wamefarijika mno kutembelewa na madaktari bingwa wa kinywa na meno kwa kuwa watoto wengi wanasumbuliwa na maradhi hayo.

Anasema ujio wao umesaidia kutoa tiba ya maradhi yanayowakabili watoto hao kwa muda mrefu sasa.

 

Kauli ya watoto

Nao watoto wa kituo hicho waliopata tiba ya kinywa na meno, wameiomba Serikali na wadau wengine wa masuala ya kinywa kuendelea kuwahudumia watoto wenye ulemavu kwa kuwa wana uhitaji mkubwa.

 

Huduma za TDA

Huduma zinazotolewa na TDA  ni pamoja na elimu ya usafi wa kinywa, uchunguzi wa meno bure, tiba ya magonjwa ya kinywa pamoja na utoaji wa dawa za meno na miswaki.

 

Kuoza kwa meno

Kuoza meno ni hali ya sehemu ya juu na ndani ya jino kutoboka.

Mbali na ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, zipo sababu nyingine zinazosababisha meno kuoza. Sababu ya kwanza ni bakteria aina ya Streptococci na Lactobacilli. Mtu anapokula chakula na kuacha mabaki mdomoni, baadaye mabaki hayo hutengeneza ‘ukoga.’

Ukoga ni utando mwembamba wa bakteria unaotokana na mabaki ya chakula mdomoni na kuota kwenye meno.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia kati ya 60 na 90 ya watoto wa shule, pamoja na takriban asilimia 100 ya watu wazima duniani, wana ukoga katika meno yao.

Bakteria wanapokula mabaki ya chakula mdomoni, hasa sukari, hukibadili chakula hicho kuwa tindikali (asidi). Tindikali hiyo huvamia tabaka gumu la juu la jino (enamel), huozesha na kulifanya liwe na matundu. Matundu hayo yanapobomoka na kuwa shimo kubwa, jino huanza kuoza. Inawezekana mtu asihisi chochote wakati huo, lakini jino linapooza kufikia sehemu zenye neva ndipo mtu anapoanza kupata maumivu makali.

Bakteria wanaotengeneza ukoga wana njia nyingine ya kuleta madhara kwenye meno. Mtu anaposukutua meno, kama ukoga hautasuguliwa na kuondolewa vizuri, unaweza kuwa mgumu na kutengeneza tabaka la vijiwe (calculus) ambayo hufanya fizi zivimbe na kuachana na meno.

Hali hiyo huleta nafasi kati ya meno na fizi ambapo mabaki ya chakula hukwama na kuliwa na bakteria wanaoweza kuathiri fizi. Mtu akipuuza tatizo hilo, tishu inayozunguka meno yake inaweza kuharibika kabisa na kufanya meno yang’oke.

 

Vyakula vinavyochangia meno kuoza

Vyakula vinavyochangia meno kuoza ni pamoja na biskuti, chokoleti, kashata, soda, pipi, keki, ubuyu wenye sukari, visheti na vyakula vingine vinavyotengenezwa kwa kuchanganywa na sukari.

 

Dalili za kuoza meno

Baadhi ya dalili au viashiria vya kuoza meno ni pamoja na alama nyeusi sehemu za pembeni za jino au kwenye nncha za kutafunia, jino kutoboka, kuvimba sehemu ya fizi au shavu upande wa jino linapouma na maumivu ya jino.

 

Njia za kuzuia meno kuoza

Mwili wa binadamu una njia ya asili ya kuzuia kuharibika kwa meno. Njia hiyo ni kutengeneza mate. Mate husaidia kulinda meno kwa kiasi fulani kutokana na bakteria. Baada ya mlo, mate yanahitaji dakika 15 hadi 45 kuondoa mabaki ya chakula na kupunguza kiasi cha asidi kwenye ukoga wa meno.

Muda huo unategemea kiwango cha sukari na mabaki ya chakula yaliyonata katika meno. Kwa hiyo, kiwango cha uharibifu unaofanywa kwenye meno kinategemea ni mara ngapi mtu anakula na kiwango cha vitafunio vyenye sukari anavyotumia, wala si kiasi cha sukari anachokula.

Kwa kuwa kiwango cha mate huwa kinakuwa kidogo mtu anapokuwa amelala, ni muhimu kabla mtu hajakwenda kulala, akasafisha meno kwa mswaki na maji safi.

 

Ushauri wa madaktari

Madaktari wa meno wanapendekeza uchunguzi wa meno uwe unafanyika walau mara moja au mbili kwa mwaka kutegemeana na hali ya meno. Watu wengi huogopa au husita kumuona daktari wa meno kwa uchunguzi kwa sababu ya gharama. Wengine wanapuuza tu kutibu meno kwa sababu hawajali.

Hata hivyo, wanashauri kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa meno, hiyo itamwepusha mtu kutumia gharama kubwa kutibu au kung’oa jino lililooza. Kwa watu wazima, madaktari wa meno hushughulika kwa kuzuia ugonjwa wa fizi zaidi kwa sababu meno yakiwa na vijiwe ni rahisi kuondolewa.

 

Njia bora ya kupiga mswaki

Kwanza madaktari wanasema kwa kuwa dawa ya meno hukwaruza na wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kuliko jino, inashauriwa kutumia kiasi kidogo cha dawa ya meno.

Pili, pinda kidogo mswaki kutoka kwenye mwisho wa fizi, kisha kwa utaratibu kabisa, piga mswaki kutoka kwenye fizi kwenda chini. Hakikisha kwamba mswaki unapigwa sehemu zote za meno, ndani na nje.

Tatu, piga mswaki pole pole kwenye nncha za meno za kutafunia. Ili kusafisha sehemu ya ndani ya meno ya mbele, shikilia mswaki wima na kisha piga mswaki kutoka kwenye fizi hadi katika sehemu ya kutafunia. Mwisho, kabla ya kumaliza, hakikisha unapiga mswaki ulimi na sehemu ya juu ya kinywa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles