25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mama Teresa: Mwanamke aliyejitoa kwa njia ya matendo, huruma

2SEPTEMBA 4 mwaka huu, Mama Teresa maarufu kama Mama Teresa wa Calcutta atakuwa rasmi mtakatifu katika hafla itakayofanyika pengine mjini Rome, Italia.

Hilo litatokea miaka 19 tangu afariki dunia mjini Calcutta, India na kuzikwa katika mazishi yaliyohudhuriwa na watu wa dini na jamii zote kabla ya serikali kumfanyia mazishi ya kitaifa kwa kutambua mchango wake kwa masikini.

Sehemu kubwa ya maisha yake yalikuwa katika mji huo wa Kolkata, ambako ni makao makuu ya Shirika lake la Masista wa Wamisionari wa Upendo, karibu na hekalu muhimu kabisa la mungu wa kike wa Kihindu na ambako mwili wake ulichomwa moto.

Ijapokuwa alikuwa Mkatoliki akiwa amebatizwa Agosti 27, 1910 siku moja tu baada ya kuzaliwa huko Skopje, (Dola la Kituruki, ambalo leo hii ni mji mkuu wa Makedonia) katika familia ya Waalbania akijulikana kama Agnes Gonxha Bojaxhiu, Mama Teresa kamwe hakujitofautisha na jamii zilizoishi eneo hilo.

Aliamini maradhi, kifo na mateso hayachagui mtu wa kumshambulia na daima aliuona utume wake wa kimissionari kama changamoto na mwaliko wa wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kukumbatia neema, huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake.

Mama Teresa alijitahidi kuhakikisha kwamba, anawaonyesha upendo wote waliokuwa wanamzunguka, akiongozwa na dhamiri nyofu.

Ni mwanamke aliyejitoa kujibu kilio cha jirani zake, kwa njia ya matendo ya huruma.

akiwa na prince dianaAlijitahidi kuhakikisha kwamba, kwa njia ya ushuhuda wa maisha, utume, watu wanatambua na kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kila mtu kadiri ya dini na imani yake.

Hakuwa mtu aliyetaka kuwashawishi waumini wa dini na madhehebu mengine kuwa Wakatoliki kadiri ya imani yake, bali kwake ilitosha kuiona ile sura ya Mungu kwa kila kiumbe.

Mama Teresa alikuwa na kipaji cha kusikiliza kwa makini na kujibu kwa wakati muafaka, changamoto kwa waumini kuendelea kujenga ndani mwao utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Hakuona ugumu wala hisia zozote kumuinua ombaomba aliyejaa ukurutu au majipu mabaya na au maradhi mengine ya kutisha iwe mwanamume au mwanamke au hata kuwachukua na kwenda nao nyumbani kwake.

Wakazi wa Calcutta walijionea jinsi alivyojitoa mhanga bila choyo, akiwa na tabasamu lake zuri la upendo na uvumilivu.

Na wakati ukiwa huwezi kuamini kuwa wakati Mfalme Alexander kutoka Macedonia alifika India katika karne ya 326 Kabla ya Kristo kuitwaa na kuwatesa watu wa India, Mmisionari huyu alitoka huko kwenda India karne nyingi baadaye kwa malengo tofauti kabisa na lile la kutesa na kutawala.

Badala ya kutawala, aliwatumikia watu wa India na kuteka kila aina ya mioyo kwa namna ambayo ni nadra dunia kushuhudia.

Zaidi ya hayo huwezi kuamini kuwa binti huyo wa Kristo alisumbuka na imani kipindi chote cha maisha yake — kama baadhi ya barua zake zilizochapishwa baada ya kifo chake zilivyofichua.

Mojawapo ya barua, kuanzia miaka ya 1959-60, mtawa huyo aliwahi kuandika katika shajara ya kiroho kuwa; “Katika roho yangu nahisi maumivu ya ajabu ya kupoteza, ya Mungu kutonipenda, ya Mungu kutokuwa Mungu, ya Mungu kutokuwepo kabisa.”

Alisema kuwa katika barua nyingine kwamba alitaka kumpenda Mungu, ‘kwa kiwango ambacho hajawahi kupendwa” lakini bado alihisi upendo wake ulikuwa haujibiwi.

Aidha, alieleza machungu na magumu anayokumbana nayo katika kuwatumikia watu wenye uhitaji.

Hata hivyo, Teresa kamwe hakuruhusu machungu hayo yawe kikwazo kwa kazi yake— ambayo ilianza mwaka 1928 nchini Ireland.

Akiwa ametangazwa mwenye heri mwaka 2003 na Papa Yohane Paulo baada ya kutambua kuwa alimponya mwanamke aliyekuwa taabani kwa ugonjwa wa Bengali, Teresa alipata uhakika kufikia hadhi ya utakatifu mwaka 2015, wakati Vatican ilipomwagia sifa kwa kuchochea kupona kwa mwanamume wa Brazil aliyeugua aina nyingi za uvimbe ubongoni.

Mbegu ya heshima hii na ukuu huu pengine ilipandwa na mama yake, Dranafile Bojaxhiu.

Baada ya kifo cha baba yake, Nikola — mkandarasi wa ujenzi na mfanyabiashara, ambaye kuhusika kwake kwa vuguvugu za kupigania uhuru nchini Albania kunahusishwa na kifo chake kwa sumu— Teresa alijiweka karibu na mama yake.

Ni mama yake aliyepandikiza mbegu ya thamani ya hisani kwa binti yake huyo aliyekuwa na umri wa miaka minane wakati huo.

Dranafile daima alimwambia binti yake kutofikiria kula ilhali kuna wengine ambao wanahitaji kuchangia chakula hicho.

Ijapokuwa familia yao haikuwa tajiri hata kidogo, mama yake daima aliwakaribisha masikini wa jiji hilo kula chakula pamoja.

Wakati huo Teresa alikuwa akiitwa Agnes — alimwambia mama yake watu hawa ni akina nani, alijibiwa baadhi ni ndugu zao, lakini wote ni watu wao wenyewe.

Hisia za huruma na utu zilipandikizwa katika moyo wa msichana huyo mdogo tangu siku hiyo.

Mwaka 1928, wakati Agnes akiwa na umri wa miaka 18 tu, aliamua kuwa mtawa na kuwa sehemu ya masista wa Loretto huko Dublin. Ni hapo ndipo alipobadili jina lake kuwa Sista Mary Teresa.

Mwaka mmoja baadaye alisafiri kwenda Darjeeling katika jimbo la mashariki la India West Bengal wakati wa kipindi cha mafunzo (novitiate period).

Baadaye alienda kufundisha Shule ya Juu ya Wasichana Mtakatifu Mary mjini Kolkata, akitumia muda mwingi kuwanoa wanafunzi masikini.

Teresa akajifunza Kihindi na Kibengali na kufikia daraja la umama kutoka usista mwaka 1937.

Lakini moyo wake haukutulia na alijihisi mwito wa Kristo na hivyo kuacha ualimu na badala yake kujitosa mitaani waliko masikini wengi.

Alitembelea mitaani ya Kolkata, akivalia vazi jeupe lenye mkanda bluu— vazi alilolivaa hadi mwisho.

Huo ulikuwa mwaka 1948, na baada ya mafunzo ya msingi kuhusu utabibu alianza safari yake ya kuwatafuta wasiotakiwa, wasiopendwa na wasiotunzwa na waliotengwa na jamii.

Hivyo, mara nyingi wanaume na wanawake wa aina hiyo walifia mikononi mwake. Huyo ndiye Mama Teresa.

Haikuchukua muda akapata makazi huko Kalighat na kuanzisha Shirika la Masista wa Wamisionari wa Upendo mwaka 1950, taasisi mpya iliyosaidia wenye uhitaji bila kujali dini yao, tabaka wala nini.

Katika kipindi cha miongo miwili iliyofuata, alifungua shule kwa ajili ya masikini na makazi kwa yatima na wenye ukoma.

Shirika hilo lilakua na wakati akifariki dunia Septamba 1997 lilikuwa na wanachama 4,000 duniani kote.

Pamoja na kusifiwa mno kwa kazi yake na hata kutwaa tuzo ya amani ya Nobel, Teresa mara nyingi alikosolewa hasa kwa kushikilia mitazamo yenye utata ya Vatican na upinzani wake wa utoaji mimba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles