24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Uhaba wa dawa unavyowatesa wagonjwa wa saratani

Mtu aliyeathirika na saratani ya kinywaMAULI MUYENJWA, DAR ES SALAAM

KUNA changamoto nyingi ambazo wagonjwa wa saratani wanakutana nazo hasa kwa wanawake ambao wana saratani ya titi.

Changamoto hizo zimesababisha wagonjwa hao kukata tamaa ya kuendelea na matibabu na kuamua kukatisha dozi na kurudi majumbani mwao.

Hali hiyo hutokea baada ya kuchoka kuhangaika kutafuta fedha za kumudu gharama za dawa huku wakizidi kunyanyasika wakiwa ugenini kwa kuja hospitali ya Ocean Road (ORCI) ambayo inashughulikia tiba na uchunguzi wa ugonjwa huo.

Changamoto kubwa ambayo waathirika wengi wanaomba kusaidiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa aina ya Chemotherapy ambayo hupewa kama tiba katika hospitali hiyo.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa Chama cha Matumaini ya Mwanamke, mmoja wa wagonjwa hao, Bihuda Shaiza, anasema huwa wanaambiwa dawa hizo ni bure lakini wanapoziulizia mara nyingi huambiwa zimeisha hivyo hulazimika kununua kwenye maduka ya nje ambako huuzwa ghali.

“Nimelipia dozi hiyo mzunguko wa kwanza kwa shida sana kwa gharama ya Sh 200,000 baada ya kuambiwa dawa hiyo haipatikani hospitalini, hapa nilipo sijui dozi ya pili na ya tatu nitaipata vipi,”anasema Shaiza.

Anaeleza kuwa alitoka Mkoa wa Tanga kufuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam baada ya ndugu aliyekuwa akimsaidia kushindwa kumudu gharama za umbali kwani ilikuwa vigumu kumhudumia akiwa huko.

Mgonjwa mwingine Mwajuma Mohamed, anasema jamii bado haijaelimika vya kutosha kuhusiana na ugonjwa huo na wanawake wengi hawaendi hospitalini kwa kuamini kuwa wanaweza kufanyiwa upasuaji na kufariki dunia.

Anadai kuwa jamii ya sasa katika baadhi ya maeneo na hasa vijijini hawaamini kama mgonjwa wa saratani ya titi anaweza kufanyiwa upasuaji na akapona.

Anaeleza kuwa hata yeye alipogundua kuwa na ugonjwa huo mwaka 2013 alipata kigugumizi kuwaambia ndugu zake akiamini hawatakubali afanyiwe upasuaji wa kuondoa titi hilo.

“Niliogopa kuwaambia kwani wapo wengine ambao wanajulikana walishafanyiwa upasuaji wakawa na hali mbaya na wapo wanaoamini kuwa hata tiba ya mionzi ina madhara.

“Lakini baada ya muda kwenda nikaona uvimbe ambao ulikuwa umejitokeza unaendelea kukua, nikafanya maamuzi ya kwenda hospitali na waliponishauri kukata nikaona sawa kwa sababu wapo ninaowajua ambao wamegoma kukata na hali zao ni mbaya, hivyo niliwashirikisha ndugu na walikubali kunisaidia,”anasema.

Mwajuma anasema bado kuna imani za kishirikina juu ya ugonjwa huo na pia wapo watu wanaoamini kuwa unaambukiza kama Ukimwi hivyo huwatenga waathirika wa saratani wakihisi wanaweza kuambukizwa.

Naye MKurugenzi wa Tanzanian Cancer Support and Hope Faundation (TCS-HOPE), Halima Kasungu, anasema wagonjwa wengi wamerudi vijijini kwao baada ya kushindwa kumudu gharama za kununua dawa hiyo kwa dozi zote pamoja na matatizo mengine wanayoyapata huko walikofikia.

“Dawa ya Chemo huuzwa ghali sana Watanzania wenye kipato cha chini wanashindwa kumudu. Wkati mwingine huuzwa Sh 300,000 hivyo wagonjwa waliokuja kufuata huduma hukata tamaa, kukatiza dozi na kuamua kurudi walikotoka,” anasema Kasungu.

Kasungu anasema ili kuweza kupunguza changamoto ya waathirika kushindwa kujikimu katika kumudu gharama za tiba ya ugonjwa,anaishauri serikali kushawishi wananchi vijijini kujiunga na bima ya afya.

“Hata wakulima wanapokuwa wamevuna na kuuza mazao yao wanaweza kujiunga na bima kwa sababu gharama za matibabu ya saratani ni kubwa sana na wengi wanashindwa kumudu ndio maana wanapata shida,” anasema.

Lakini ni wagonjwa wengi ambao wangeweza kutambua ugonjwa huo mapema kabla ya kufikia hatua mbaya na kuweza kutibiwa wakapona tatizo ni elimu kwa wanawake wengi kugundua ugonjwa huo mapema pamoja na juhudi za serikali kutoa elimu.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Faundation For Care in Tanzania, John Reiling kwa kushirikiana na Chuo cha saratani cha Minnessota kilichopo Marekani, anasema watafungua kituo cha uchunguzi na tiba ya magonjwa ya saratani katika hospitali ya rufaa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro (KCMC).

Reiling anasema kituo hicho kitaanza na kutoa matibabu na kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo kwa watoto na baadae watafanya kwa watu wazima.

“Ili kuweza kuzuia changamoto za kutibu ugonjwa huu ni lazima kuwe na mpango kabambe wa uchunguzi kwa watoto na watu wazima ili kuweza kutoa tiba mapema wanapogundulika na kuzuia msongamano hospitalini.

“Mpaka sasa tumefanikiwa kupata Dola za Kimarekani milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na bado tunatafuta fedha kwa wadau mbalimbali ili kukifanikisha,” anasema.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya wakati wa Siku ya Saratani Duniani, wagonjwa wa saratani wanazidi kuongezeka kila mwaka.

Takwimu toka ORCI zinaonyesha kuwa wagonjwa wapya wanaofika kutibiwa wanaongezeka kwa kasi toka wagonjwa 2,807 mwaka 2006 hadi kufikia 5,529 mwaka 2013.

Ni asilimia 70 ya wagonjwa wa saratani hupoteza maisha katika nchi zinazoendelea, na katika bara la Afrika lenye watu zaidi ya milioni 804, asilimia 12.4 wanapata saratani kabla ya kufikia umri wa miaka 75 na asilimia 90 wanapata ugonjwa huo wakiwa na umri chini ya miaka 40.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles