ISTANBUL, UTURUKI
MCHEZO wa wapinzani kati ya Galatasaray dhidi ya Fenerbahce wa Ligi Kuu nchini Uturuki uliahirishwa kutokana na mlipuko wa bomu.
Mchezo huo ulitakiwa kupigwa juzi, lakini kutokana na bomu ambalo lililipuka Jumamosi na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi zaidi ya 30, Shirikisho la Soka nchini humo (TFF) lilitangaza kuahirishwa kwa mechi hiyo.
Jeshi la Polisi nchini humo linaendelea kufanya uchunguzi kwa ajili ya kuwatafuta wahusika wa tukio hilo.
Mchezo huo ulivunjwa saa 2 kabla ya kuanza, huku shirikisho likidai kwamba ni kwa ajili ya usalama wa raia.
“Nchi imepoteza watu watano kutokana na mlipuko wa bomu, hii ni hali ya kusikitisha, lakini ratiba ya mchezo huo itatangazwa rasmi mara baada ya hali ya usalama kukaa sawa,” waliandika TFF.
Hata hivyo, klabu ya Galatasaray, imewataka mashabiki wake kuwa wavumilivu hadi pale hali ya usalama itakapokuwa sawa.