25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Majaji ondoeni tuhuma za rushwa mahakamani-Dk. Mpango

*Ahimiza kuendelea kuwa wabunifu

Na Clara Matimo, Mwanza

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango amewataka Majaji nchini kuendelea kuwa wabunifu na kuimarisha uwezo wa mahakama kwa kutumia tehema ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa majaji na watumishi wa mahakama.

Pia amewataka kuondoa tuhuma za rushwa dhidi ya muhimili wa mahakama walizonazo wananchi ili wajenge imani kwa mahakama huku akiwataka watumishi wa mahakama kutoa haki kwa kila mwananchi anayehitaji huduma kutoka kwao bila kupendelea.

Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango (aliyesimama juu ya gari) akizungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, ambapo pia alisikiliza changamoto zao ikiwemo uhaba wa maji na kuwaahidi kwamba miradi inayotekelezwa itakamilika kwa wakati.

Dk. Mpango ameyesema hayo jijini hapa leo Aprili 12, 2023 wakati akifungua mkutano wa tathmini ya utendaji wa mapitio ya nusu ya kwanza ya mpango mkakati wa mahakama 2020/2021 hadi 2024/2025 kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambao utasaidia kuongeza ufanisi wakati wa utekelezaji wa shughuli za mahakama.

“Endeleeni kutoa mafunzo kwa watumishi hasa wa kada ya chini na kuwajengea uwezo wa kutoa huduma kwa njia za kidigitali, mimi naamini hii itasaidia kuwahudumia wananchi wengi zaidi na kujibu maswali pamoja na kutatua changamoto zao kwa wakati, serikali itaendelea kuboresha utendaji kazi wa mahakama ili kuiwezesha kuendelea kutoa haki kwa wananchi na kuimarisha mnyororo wa utoaji haki.

“Kuhusu tuhuma za rushwa, sisi tunapita kwenye mikoa mbalimbali kutembelea wananchi bado wanahisi kuna rushwa katika mfumo wa mahakama kwa hiyo ni lazima mahakama izifanyie kazi hisia hizo tumieni mkutano huu kufanya tathmini ya mianya na viashiria vya rushwa na kuchukua hatua ili kujenga imani ya wananchi katika muhimili huu muhimu wa mahakama,” amesisitiza Dk. Mpango.

Wananchi wa Kata ya Kisesa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wakimsikiliza Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango(hayupo pichani).

Ameeleza kwamba ufanisi wa shughuli za utoaji haki nchini ni nguzo muhimu ya kulinda amani na utulivu uliopo, kukuza utawala wa sheria pamoja na shughuli za kiuchumi, biashara na uwekezaji hivyo majaji waendelee kufanya kazi kwa uadilifu ili kuwawezesha watanzania kupata haki kwa mujibu wa sheria, ucheleweshwaji wa mashauri unaongeza gharama si tu kwa wadau bali hata kwa uchumi wa taifa hivyo ni wajibu wa mahakama kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mahakama kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za utendaji kazi wa muhimili wa mahakama nchini hususan kwa kuiwezesha mahakama kifedha katika kutekeleza majukumu yake kwani muhimili huo ni moja ya nguzo ya kudumisha amani na utamaduni wa nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema mkutano huo ni muhimu sana katika kuhakikisha utendaji kazi wa mahakama unaimarika mkoani humo huku akiwaomba waandaaji kuendelea kufanyia mikutano yao mkoani kwake kila mwaka ili washiriki kuchangia ukuaji wa uchumi kwa kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya mkoa huo ikiwemo kisiwa cha saa nane.

Naye, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibahim Juma amesema Novemba 10,2014 walifanya mkutano ambapo walitengeneza mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia 2015/2019 uliotoa dira ya mwelekeo wa mahakama katika kufikia lengo la kuwa na mahakama iliyokaribu na wananchi na inayotoa huduma kwa haki ili kukabiliana na changamoto zilizokuwa zinaukabili mfumo wa utoaji haki ikiwemo ucheleweshaji mkubwa katika utatuzi wa migogoro,vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili ili kuhakikisha wananchi wanaridhika na huduma wanazozitoa.

“Katika kuboresha huduma tunazozitoa tumetunga kanuni mpya zaidi ya 75 katika kamati mbalimbali tunachopaswa kujiuliza je ndani ya hizo kanuni zimeleta mabadiliko gani?,” amehoji Prof. Juma.

Akiwa Mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia April 11 hadi 12, 2023 Makamu wa Rais Dk. Mpango leo pamoja na kufungua mkutano huo pia amezungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu Wilaya ya Ilemela na Kisesa iliyopo Wilayani Magu ambapo alisisitiza wazazi, walezi viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika malezi ya watoto ili wakue katika maadili mema ya kitanzania pamoja na kuwapeleka shule wapate elimu kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles