27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Atakaye kula fedha za Boost Ileje kuwajibishwa

Na Denis Sekonde, Songwe

BAADA ya Serikali kutoa fedha zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kwa shule za msingi nane wilayani Ileje mkoani Songwe wasimamizi wa miradi hiyo wametakiwa kujiepusha na ufujaji.

Agizo hilo limetolewa Aprili 11, 2023 na Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi wakati akizungumza na walimu wakuu wa shule zitakazotekeleza mradi huo, maafisa elimu kata, na baadhi ya wakuu wa idara ya elimu msingi, manunuzi, mipango, fedha, ardhi na mazingira.

Baadhi ya Walimu Wakuu, Waratibu Elimu Kata na Wakuu wa Idara wakisikiliza kikao hicho.

Mgomi amewataka viongozi hao kusimamia miradi hiyo kwa uaminifu na kujiepusha na tamaa ya fedha kwenye miradi ya boost ambayo serikali imetoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ambayo imekuwa ni kilio kwa muda mrefu.

Mgomi amesema serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni 1.5 wilayani humo kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa, vyoo na nyumba ya walimu hivyo ni jukumu la kila mkuu wa Idara kusimamia na si kuiachia idara ya elimu msingi pekee yake.

“Jukumu la kusimamia mradi huo ni jukumu la kila mkuu wa idara katika halmashauri hiyo kwa kupewa mradi wa kusimamia ili ikamilike kwa wakati kulingana na ukomo wa Juni 30,2023,” amesema Mgomi.

Mgomi amesisitiza kuwa kila wiki ofisi yake ipokee taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na changamoto zinazokwamisha Ili kuzitafutia ufumbuzi kwa muda kulingana na ukomo uliotolewa.

Afisa Elimu Msingi wilayani humo, Fikiri Mguye amebainisha baadhi ya shule zilizonufaika na mradi huo ni shule ya msingi Ibezya imeingiziwa Sh milioni 150 kwa ajili ya madarasa sita na milioni 12 kwa ajili ya matundu sita ya vyoo, Mtula milioni 100 vyumba vinne vya madarasa na matundu sita  yavyoo, shule ya msingi Ibaba milioni 69 madarasa mawili ya elimu msingi awali, shule ya msingi Ikumbilo milioni 347 kwa ajili ya kujenga shule mpya ya mkondo mmoja.

Mguye ameongeza kuwa shule ya msingi Chitete Sh milioni 347, shule ya msingi Ilulu imepata Sh milioni 162 ambapo Sh milioni 150 zitajenga madarasa sita na Sh milioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo matundu sita, shule ya msingi Sange imepata Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya mfano vya elimu msingi awali na Sh milioni 100 kwa ajili ya nyumba ya walimu.

“Ujenzi huo unapaswa kujengwa Kwa kuzingatia muongozo hivyo kama wilaya tunapaswa kushirikiana kusimamia ujenzi huo ili thamani ya mradi iendane na fedha iliyotolewa ili kuepuka hoja za mkaguzi mkuu wa serikali,” amesema Mguye.

Kwa upande wake Afisa Elimu kata ya Lubanda, Adamu Mpuna ameomba wasimamizi wa mradi kwenye shule kuanza na wahandisi kufika eneo la mradi mapema kutoa maelekezo Kwa mafundi namna ya kujenga mradi kwa viwango vinavyotakiwa.

Ikumbukwe kuwa mradi wa BOOST umekuja kwa ajili ya kuinua elimu ya awali na msingi ambao unatekelezwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa fursa katika ufundishaji na ujifunzaji bora was elimu ya awali na msingi Tanzania bara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles