22 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

Woga bado tatizo mapambano ukatili wa kijinsia

Na Derick Milton, Simiyu

Licha ya serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza mapambana dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, tatizo la woga miongoni mwa waathirika bado ni kikwazo kikubwa katika mapambano hayo.

Wanawake wakiwa miongoni mwa waathirika zaidi wa vitendo hivyo, wengi wao hasa maeneo ya vijijini wamekubwa na woga na kushindwa kutoa taarifa katika mamlaka husika pindi wanapokumbana na vitendo hivyo.

Hayo yamebainishwa jana na Mawakala wa mabadiliko ya tabia ngazi ya jamii katika Wilaya ya Bariadi, wakati wa kampeini ya kuimarisha usawa wa kijinsia katika kata za Sapiwi na Dutwa inayoendeshwa na Shirika la Mass Media la Mjini Bariadi.

Mawakala hao walisema kuwa changamoto wanayokumbana nayo hasa kutoka kwa wanawake ni woga, ambapo wengi wao uhofia kutengwa na familia zao ikiwa watagundulika wametoa taarifa za kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Kuna mwanamke mmoja yeye alikuja kwangu kuniambia vitendo anavyofanyiwa na mme wake, baada ya kumsikiliza nikamuuliza sasa tupeleke hizi taarifa kwenye mamlaka, akataa akasema alikuwa ananiambia tu, baadaye akaanza kunikana kuwa hajaniambia,” anasema Robert Madelya Wakala.

Naye Mkwaya Hebu wakala alisema kuwa matukio mengi ambayo amekutana nayo ni wanawake kufanyiwa unyanyasaji wa kiuchumi na waume zao, huku wengi wao wakishindwa kutoa taarifa.

“Huku kwetu wanawake wanafuga sana hasa kuku pamoja na kujihusisha na kilimo, ikifika wakati wa mavuno hizo mali siyo zao tena, hata kuku wanaume ndiyo wanauza na kutumia pesa zote,” anasema Hebu.

Aliongeza kuwa wengi waliofanyiwa vitendo hivyo, hawataki taarifa zao kupelekwa katika vyombo vya kisheria au serikalini wakihofia kutengwa na familia zao au kufukuzwa na waume zao.

Mkurugenzi wa Mass Media Frank Kasamwa akizungumza kwenye Kampeini hiyo inayotekelezwa chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation For Civil Society (FCS) alisema kuwa ni wakati wa jamii kuacha woga na ili matukio hayo yaweze kukomeshwa.

“Hatuwezi kukomesha vitendo hivi ikiwa wahusika wenyewe wanaendelea kuficha matukio haya ndani, vitendo hivi vitolewe taarifa ili kuweza kukomeshwa, na wazazi adhabu kwa watoto wetu ziwe na vipimo,” alisema Kasamwa.

Ofisa Ustawi wa Jamii Wilayani humo Womdenge Kalingoji aliwataka wananchi hasa wanawake na watoto kutoa taarifa kwenye ofisi yeyote ya serikali au kwa kiongozi yeyote wa serikali pindi wanapofanyiwa au kukutana na vitendo hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,284FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles