NYOTA wa mbio za magari ya Langalanga, Lewis Hamilton, yupo kwenye uchunguzi na polisi wa New Zealand baada ya kukutwa akijipiga ‘selfie’ wakati akiwa anaendesha pikipiki wiki hii ambayo inatarajia kuanza kwa michuano ya Australia Grand Prix.
Hamilton alikamatwa siku moja kabla ya kuanza kwa michuano hiyo leo katika jiji la Melbourne, ambayo anatakiwa kutetea ubingwa wake aliopata msimu uliopita.
Hata hivyo, kitendo hicho ni moja ya uvunjaji wa sheria ya mwaka 2009 ya nchi hiyo ambayo inakataza kutumia simu wakati wa kuendesha vyombo vya moto.
Ingawa baada ya kukamatwa kwa nyota huyo polisi hawakuchukua hatua yoyote ya kisheria kutokana na kutokuwa na ushahidi wa kutosha, lakini walimkanya kutumia simu akiwa anaendesha gari au pikipiki.
Tukio hilo ni miongoni mwa rekodi mbaya dhidi ya nyota huyo ambapo mwaka jana akiwa Monaco aliwahi kusababisha ajali iliyoweza kuharibu gari la Zonda Supercar lenye thamani ya pauni milioni 1.
Pia aliwahi kulipa faini ya pauni 300 kwa kuendesha gari mwendo wa kasi kinyume cha sheria mwaka 2007 akiwa Ufaransa, alifungiwa leseni yake kutokana na tukio kama hilo.