Na Asifiwe George, Dar es Salaam
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Dk. Juma Mwapachu, ametangaza kurejea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akieleza namna Rais Dk. John Magufuli atakavyoweza kukijenga chama hicho na kukirudisha katika misingi ya demokrasia na haki.
Hatua hiyo ameichukua ikiwa imepita miezi mitano tangu alipotangaza kujiengua na chama hicho Oktoba 13, mwaka jana na na kueleza kutojiunga na chama chochote cha siasa.
Baada ya uamuzi huo, Balozi Dk. Mwapachu alikabidhi kadi yake ya uanachama kwenye ofisi ya CCM Kata ya Mikocheni, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Dk. Mwapachu alisema ana imani kwamba Tanzania hivi sasa imeingia katika zama mpya, na kitabu kipya kimeandaliwa na kinazidi kufunuliwa na Rais Magufuli.
“Naamini kuwa zama hii mpya itaona uzinduzi wa kitabu kipya kuhusu uongozi ndani ya CCM, naamini kwa dhati kabisa kwamba Rais Magufuli atakaposhika hatamu za kuongoza CCM, atakirejesha chama hiki kipya, ataimarisha CCM na kukirejesha katika misingi ya kidemokrasia.
“Na itabidi iwe hivyo kwa sababu ushindani wa kisiasa nchini umeimarika, CCM haina budi na italazimika kufungua milango upya ili kirejeshe hadhi yake kama chama cha wakulima na wafanyakazi.
“Yaliyopita si ndwele tugange yajayo, kwa kiasi fulani itikadi ya msemo huu ni kiini kimojawapo cha uamuzi ambao nimeuchukua, wa kurejea katika chama, chama changu tangu mwaka 1967.
“Niko tayari kushiriki katika ujenzi wa fikra mpya za kukiimarisha chama chetu,” alisema Dk. Mwapachu.
Alisema yaliyotokea wakati wa harakati za kumpata mgombea urais ndani ya CCM na baadaye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, kwa hakika kwake si ndwele bali ni maradhi ya kibinadamu yanayotibika kwa urahisi.
Dk. Mwapachu alisema haoni haja au umuhimu wa kurejea mazingira hayo, na hasa ikitambilika kwamba hakujiunga na chama kingine chochote cha siasa.
Alisema tangu Uchaguzi Mkuu umalizike na matokeo kufahamika, amepitia kipindi kigumu cha kupima na kutafakari mustakabali wake kisiasa.
Dk. Mwapachu alisema katika wiki saba zilizopita amekuwa na mawasiliano na Ofisi ya Kata ya Mikocheni kuhusu vipi angeweza kukubaliwa kurejea uanachama wa CCM.
Alisema kiini na msingi wa kurejea CCM ni kutokana na mafundisho na hekima za Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, ambapo aliwahi kutamka kwamba kila zama na kitabu chake.
Dk. Mwapachu alisema alikuwa akifafanua utofauti wa misingi na mielekeo ya uongozi pale yanapotokea mabadiliko ya viongozi na demokrasia, maana yake ni kwamba viongozi wapya hupima hali na mazingira halisi ya nchi na hata yale ya vyama vyao vya siasa ambapo wengi wao hufungua kurasa mpya zinazokidhi matarajio na matumaini ya watu.
Alisema kutokana na kurejea kwake, anatoa kiasi cha Sh milioni moja kwa ajili ya kuboresha ofisi ya CCM Mikocheni ili iwe katika hadhi ya Mikocheni.
Alipoulizwa na waandishi kuhusu kurejea kwake katika chama hicho kama kunatokana na biashara zake kushikiliwa, alikanusha na kusema kuwa hana biashara yoyote bali anajishughulisha kwa nguvu zake na yeye ni Rais wa Societies of Nation Development.
Balozi Mwapachu alisema kuwa siku 10 zilizopita alikutana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM ambaye kwa sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, na kumweleza dhamira yake ya kurejea ndani ya CCM.