Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Shirika la Aga Khan Foundation leo Juni 30, mwaka 2022 limetoa ruzuku ya Sh milioni 169,177,000 kwa vikundi 90 vya huduma ndogo za fedha lengo likiwa ni kuwainua wajasiriamali wadogo na kuwajengea uwezo ili waweze kuboresha biashara zao.
Kaimu Mkurugenzi Mkazi, wa Aga Khan Foundation, Simon Moikain, amesema ruzuku hizo wamezitoa kupitia mradi wanaoutekeleza wa kuvisaidia vikundi vya huduma ndogo za fedha kutokana na changamoto za UVIKO-19 ambao unatekelezwa katika nchi tano ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Madagaska na Msumbiji.
Amesema mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Aga Khan Foundation kwa kushirikiana na European uonion huku akifafanua kwamba hapa nchini unatekelezwa katika mikoa ya Mwanza Dar es Salaam, Mtwara na Lindi.
“Lakini katika kipengele cha ruzuku ya kuweka na kukopa kiko Mwanza katika halmashauri za jiji hilo, Buchosa, Ilemela,Magu na Sengerema, kwa mikoa mingine ni Lindi na Mtwara pekee, tunawezesha vijana, tunawafundisha masuala ya ujasiriamali na uwezo wa kusimamia biashara na wachache ambao wataonyesha ubunifu kwenye uandaaji na uendeshaji wa biashara,”amesema Moikain.
Mratibu wa mradi huo, Japhet Wangwe amesema vikundi vyote vilivyopo kwenye mradi huo vitapata ruzuku ya zaidi ya Sh Milioni 169 na vinaanza rasmi kazi kuanzia Juni 30 mwaka huu na kwamba mradi upo kwenye mfumo wa hisa ambazo zitaendeshwa kwa kutumia simu katika kufikia malengo.
Amesema mradi huo unafanya kazi na wajasiriamali hadi sasa wanao vijana 100 kutoka Mkoa wa Mwanza ambao watajengewa uwezo wa kuboresha biashara zao ili waweze kujiinua na kuwaajiri wenzao ndani ya jamii.
“Mhe Mkuu wa Mkoa tuliandaa utaratibu wa kupata vikundi hivi na tunashukuru ofisi za maafisa maeneleo za Halmashauri na Mkoa kwa usaidizi na hapa leo tupo na vikundi vya wawakilishi 90 ambavyo ndivyo vinaenda kupokea ruzuku hizi,” amesema Wange.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ametoa rai kwa vikundi vilivyofuzu kupata ruzuku hiyo kwa ajili ya kuendesha biashara katika kupambana na athari zitokanazo na ugonjwa wa Uviko 19 kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kukithi nia ya mradi huo.
“Kipekee kabisa naomba nimshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia awamu ya Sita ya uongozi wake kwa kuendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbalimbali ikiwemo Umoja wa Ulaya ambao pia wamefadhili mradi huu wakishirikiana na Shirika la Aga Khan Foundation.
“Hii ni fursa kubwa sana kwa mkoa kwa kupatiwa usaidizi wa kitaalamu na kifedha katika kuhakikisha wananchi wetu wanajengewa uwezo hivyo ni lazima mdhihirishe kwamba kule kuaminiwa kwenu kunaleta taswira kwamba Mkoa wa Mwanza mradi ukileta unatekelezeka.” Mhandisi Gabriel,”amesema na kuongeza.
“Naomba niwasihi wanavikundi wote kuwa ruzuku hizi sio kwa ajili ya kufanyia sherehe, kununulia nguo mpaya au kujengea nyumba, mnapewa fedha kwa ajili ya kuendesha biashara zenu katika kujiinua kutoka kwenye umasikini,”amesema Mhandisi Gabriel.