26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

TARURA kufungua KM 1,680 za mtandao wa Barabara Sikonge

Na Allan Vicent, Tabora

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Sikonge Mkoani Tabora wanatarajia kufungua mtandao wa barabara wenye urefu wa km 1,680 katika maeneo mbalimbali katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA wilayani humo, Eng.Eligidius Kaselwa alipokuwa akiongea na gazeti hili jana Ofisini kwake ambapo alisema kwa sasa halmashauri ya wilaya hiyo ina mtandao wenye urefu wa km 922.7 zilizohakikiwa na kutangazwa kwenye gazeti la serikali.

Alisema km 148 zimepimwa na kuwekwa katika mapendekezo ya uhakiki ili ziweze kuongezwa katika mtandao huo na barabara nyingine bado hazijaingizwa katika mfumo huku akibainisha kuwa upitikaji wa barabara zote ni wa wastani.

Alifafanua kuwa hadi sasa wamejenga km 3.1 za lami, km 262.88 za changarawe na km 656.48 za udongo na katika mwaka huu wa fedha wanatarajia kuongeza barabara za lami hadi kufikia km 3.5, changarawe km 328 na za udongo zitapungua hadi km 581.

Mhandisi Kaselwa aliishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaongezea fedha za matengenezo ya barabara kutoka bajeti ya awali ya sh mil 829.8 hadi kufikia bil 4.19.

‘Tunaishukuru serikali kwa kututengea sh bil 4.19 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya barabara na matumizi ya Ofisi, hii bajeti ni mkombozi kwa wananchi wa Sikonge kwa kuwa itawezesha barabara nyingi kutengenezwa’, alisema.

Alifafanua ongezeko hilo kuwa ni sh mil 820 za matengenezo ya kila mwaka, sh mil 500 za Majimbo, sh bil 1 za tozo na sh bil 1.8 za matengenezo maalumu ya barabara inayounganisha kata ya Nyahua na Makao Makuu ya wilaya.

Kaselwa alieleza kuwa jumla ya mikataba 4 imesainiwa na Wakandarasi kwa ajili ya matengenezo ya barabara 18 kupitia fedha za Mfuko wa Barabara na mikataba mingine 5 kwa ajili ya matengenezo ya barabara 16 kwa kiwango cha changarawe.       

 Alibainisha kuwa katika mwaka huu wa fedha barabara zote zilizokuwa hazipitiki zitatengenezwa na nyingine mpya zitafunguliwa ili kurahisishia wananchi usafirishaji mazao yao kutoka shambani kwenda kwenye masoko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles