Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
RIPOTI ya awali ya Utoaji wa Huduma za Kipolisi (PDB) inayosimamia usalama wa raia na mali zao, inaonyesha Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni unaongoza kwa vitendo vya uhalifu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Dar es Salaam jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, alisema ripoti hiyo imetolewa ili kupanga mikakati mipya ya kupambana na vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo Kinondoni.
Alisema kutokana na hali hiyo, jeshi hilo limejipanga kuhakikisha vitendo hivyo vinakwisha ili wananchi waishi kwa amani na utulivu.
“Tulifanya utafiti na kubaini Kinondoni inaongoza kwa vitendo vya uhalifu, hali iliyotufanya tushirikiane na wadau mbalimbali ili kuhakikisha tunakomesha vitendo hivi.
“Kwa majaribio tumeanza na Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, tutaongeza ofisi za huduma za kipolisi,” alisema Mangu.
Aliongeza kuwa hadi sasa wamefungua vituo vya kanda za kipolisi 37 maeneo mbalimbali ya mkoa huo ambavyo vitakuwa na askari wa kutosha, ambao watakuwa na silaha kwa ajili ya kufanya doria.
Alisema askari hao watakuwa tayari kupambana na uhalifu wa aina yoyote utakaojitokeza.
Mangu alisema ripoti hiyo imetolewa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao unahitaji kutekelezwa kwa vitendo.
Aliwataka askari wa jeshi hilo kila mmoja kutimiza majukumu yake kulingana na nafasi yake ili waweze kupambana na uhalifu.
Alisema endapo Serikali itatoa fedha za kutosha, kazi hiyo itaendelea katika mikoa mingine ya kipolisi ya Ilala na Temeke na baadae kusambaa nchi nzima.