Patricia Kimelemeta na Florian Masinde
MSHINDI wa kwanza kitaifa, Butogwa Shijja kutoka Shule ya Sekondari Canosa ya jijini Dar es Salaam, amesema siri kubwa ya mafanikio yake ni kusoma kwa bidii bila kuchoka.
Alisema malengo yake ni kusoma katika ya vyuo vikuu bora duniani ili baadaye awe daktari asaidie wananchi.
Akizungumza na MTANZANIA shuleni hapo jana, Butogwa alisema lengo kubwa alilojiwekea katika maisha yake ni kuwa daktari.
Alisema alikua akisoma kwa bidii ili aweze kutimiza malengo yake hayo na baadaye aweze kutoa mchango mkubwa kwa jamii.
“Ndoto zangu ni kuwa daktari kwa sababu napenda kuwasaidia wananchi, ndio maana nimesoma kwa bidii,”alisema Butogwa.
“Hata wazazi wangu niliwaambia nitasoma kwa bidii ili niweze kupata udhamini wa kwenda kusoma kwenye vyuo kumi bora duniani,”alisema.
Kwa upande wake, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Angela Shijja alisema alikuwa na matumaini makubwa kwamba mwanae angefaulu kutokana na bidii ya kusoma aliyokuwa nayo.
“Ninaamini mwanangu anaweza kufikia malengo aliyokusudia ya kupata udhamini wa kusoma chuo bora duniani ili aweze kuwa daktari.
“Mkakati wetu kama wazazi ni kumwendeleza binti yetu ili aweze kutimiza ndoto zake alizojiwekea,” alisema.
Akizungumzia ufaulu huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Sister Irene Nakamanya alisema kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na juhudi binafsi katika masomo.
“Pale anapoona hajaelewa huwa anawatafuta walimu ili waweze kumwelewesha vizuri.
“Butogwa alikua na tabia ya kuwasumbua walimu ili waweze kumwelewesha vizuri pale ambapo anaona hajaelewa lakini pia alikuwa na bidii katika mitihani mbalimbali iliyotolewa shuleni hali iliyochangia kufaulu,”alisema.
Akizungumzia ufaulu wa shule hiyo mkuu huyo alisema siri ya shule yake kutoa mwanafunzi wa kwanza na wa tatu katika 10 bora ni mapenzi ya Mungu pamoja na juhudi za ziada za walimu,wazazi na wanafunzi wenyewe.
“Walimu wangu wamekua na moyo wa kujitolea wakati wa kufundisha,hali iliyosaidia wanafunzi kusoma kwa bidii,”alisema Nakamanya.