24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri awachimba mkwara Polisi

Charles-Kitwanga-1NA ASIFIWE GEORGE, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amewatahadharisha askari polisi wanaowarubuni wananchi wasishiriki marudio ya Uchaguzi Mkuu visiwani Zanzibar kuacha mara moja tabia hiyo.

Kitwanga alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi.

Alisema kuna baadhi ya askari polisi huko Zanzibar wanawarubuni wananchi ili wasishiriki kupiga kura, huku akisisitiza kuwa atakayebainika akifanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.

“Yapo pia malalamiko juu ya baadhi ya askari na maofisa wachache wanaotumia nembo za polisi vibaya kwa kuwabambikizia kesi wananchi, kuomba na kupokea rushwa, kuchelewa kufika eneo la tukio hata kama ni umbali mfupi, kula njama na watuhumiwa na hivyo kuharibu vielelezo vya kesi,” alisema waziri huyo.

Aidha alisema wapo baadhi ya askari ambao  wamekuwa wakichelewesha upelelezi wa kesi, kutowajali wateja na kwamba watu hao hawatavumiliwa kwani wamekuwa ni kero katika jamii.

“Nina imani kila kiongozi akijiepusha katika kulinda na kuendekeza mambo ya ovyo na kuwasimamia anaowaongoza ipasavyo, malalamiko ya aina hiyo yatapungua,” alisema Waziri Kitwanga.

Kuhusu ajali za barabarani, Kitwanga alisema tatizo hilo limeendelea kukua siku hadi siku, hasa zile zinazohusisha pikipiki maarufu kama bodaboda.

Kutokana na hilo, alisema anaunga mkono hoja na harakati zinazofanywa na Kitengo cha Usalama Barabarani kwa kutoa elimu ya kukabiliana na ajali hizo.

“Katika Jiji la Dar es Salaam kumekuwa kukiripotiwa ajali nyingi zinazohusisha bodaboda ambazo nyingi zinasababisha vifo au ulemavu kwa madereva na hata abiria.

“Mbali na kuhusika katika ajali za barabarani, bodaboda pia zimekuwa zikihusika katika matukio ya kihalifu, hasa unyang’anyi wa kutumia silaha, nina imani kupitia mkutano huu tutapata suluhisho la tatizo la uhalifu wa kutumia silaha kwa kutumia pikipiki,” alisema Kitwanga.

Aidha waziri alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja na kwamba amekuwa akisikia taarifa za kukamatwa kwa mirungi na bangi, lakini dawa za kulevya za viwandani hazikamatwi.

“Ninawakumbusha kudhibiti mitandao ya dawa za kulevya za viwandani na tutapima ufanisi wenu wa kazi kwa kuangalia uhalifu wa aina zote, hasa eneo hili la dawa za kulevya, hii ni vita kubwa na inahitaji umakini wa hali ya juu,” alisema Kitwanga.

Katika mkutano huo, Kitwanga aliwataka makamanda wa mikoa kuweka mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu katika maeneo yao ili kupunguza uwezekano wa wahalifu kukimbilia maeneo mengine pale wanapofanya uhalifu.

“Kamanda wa Mkoa wa Pwani, Tanga na Morogoro mnapaswa kuwa makini katika maeneo yenu. Nimeitaja mikoa hiyo kwa sababu imekuwa na matukio ya kihalifu yanayojirudia mara kwa mara,” alisema.

Waziri huyo alisema takwimu zinaonyesha kuwa kipindi cha mwaka 2015 makosa makubwa yaliyoripotiwa yalikuwa 68,814 ikilinganishwa na 70,153 yaliyoripotiwa mwaka 2014 ambayo ni pungufu ya makosa  1,339 sawa na asilimia 1.9.

Kwa upande wake, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema kwa sasa wanaendelea kujipanga kuimarisha amani na utulivu kwenye marudio ya Uchaguzi wa Zanzibar.

“Tunaomba ushirikiano kwa wananchi na wadau wote wa uchaguzi ili tuweze kuweka mazingira mazuri na salama kwa wananchi  kutumia haki yao ya kuchagua viongozi,” alisema.

Aidha IGP Mangu alisema uhalifu umepungua, lakini zipo changamoto nyingi za uhalifu ikiwamo kushughulikia matukio ya migogoro ya ardhi, hasa inayohusisha wafugaji  na wakulima ambayo imesababisha mauaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles