NA WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital
KITENDO cha bondia Francis Miyeyusho, kutamba kuwa hakuna bondia wa kumpiga katika kambi zote za Mabibo, Manzese na Mburahati, mashabiki wa ndondi wa mitaa hiyo wameamua kuungana kuhakikisha bondia huyo anachezea kichapo Oktoba 30, mwaka huu atakapopanda ulingoni dhidi ya Adam Kipenga.
Miyeyusho ambaye anatoka kambi ya Kinondoni, watazichapa na Kipenga wa Manzese katika pambano la usiku wa Mwana Ukome Derby ya Dar ea Salaam kwenye Uwanja wa Kinesi.
Mabondia hao wametambiana leo Septemba 17, mbele ya mashabiki wao wakati wa utambulisho kwenye viwanja vya Las Vegas, Mabibo, jijini Dar es Salaam.
“Miyeyusho anasema hakuna bondia wa kumpiga kutoka Manzese,Mabibo wala Mburahati, lakini niwaambie mashabiki wangu kuwa safari hii hatoboi,” ametamba Kipenga huku akishangiliwa na mashabiki waliojitokeza hushudia utambulisho huo.
Kwa upande wake Miyeyusho ambaye alichelewa kufika eneo la tukio, amesema yeye hana maneno mengi kwa sababu kazi yake wanaijua.
‘Derby’ nyingine ya kibishi ya Mwana Ukome ambayo ndio pambano kubwa itawakutanisha wababe wa Mabibo na Manzese, Iddi Pialari na Ramadhani Shauri.
Mabondia wengine watakaopanda ulingoni siku hiyo ni kutoka Jeshi la Wananchi (JWTZ), Selemani Kidunda, Ismail Galiatano,George Bonabucha na Grace Mwakamele.
Wengine ni Hassan Ndonga, Ramadhani Idd, James Kibazange na Ally Ngwando.
Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Promota wa mapambano hayo, C.E.O wa PeakTime Media, Kapteni Selemani Semunyu, amesema kutokana na kukubali matakwa ya mashabiki wake ngumi, ameamua kuhamishia michezo hiyo Uwanja wa Kinesi badala ya Beach Kidimbwi.
Amesema anataka kuwapa mashabiki wake kile wanachotaka, huku akikaribisha wadhamini kusapoti mchezo huo.