Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Shirikisho la Soka kwa Watu wenye Ulemavu Tanzania(TAFF), limesema linahitaji kiasi cha fedha sh milioni 625 ili kufanikisha kuandaa michuano ya Afrika ya watu wenye ulemavu iliyopangwa kuanza Novemba 25-Desemba 5, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kutokana na uhitaji wa fedha hizo, shirikisho hilo limewaomba wadau kujitokeza kuwa kusaidia ili kufanikisha maandalizi ya michuano hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Dar es Salaam Katibu Mkuu wa TAFF,Peter Sarungi, amesema mashindano hayo ni maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia inayotarajia kufanyika mwakani nchini Uturuki.
Amesema mashindano hayo yana umuhimu mkubwa na yanahitaji maandalizi mazuri kutokana na nchi zinazotarajiwa kushiriki.
“Nchi zinazokuja kushiriki zimebobea katika mpira wa miguu ambazo ni Ghana, Liberia Angola, Rwanda, Cameroon, Ethiopia, Gambia, Uganda, Misri, Sierra Leone, Morroco, Togo mwenyeji Tanzania Bara, lakini tunafanya mchakato wa kuhakikisha Zanzibar nayo inahusika,” ameeleza Sarungi.
Naye Ofisa Habari wa TAFF, Masau Bwire, amesema fedha zinazohitajika ni nyingi, pamoja na kwamba Serikali imechangia lakini si kiasi chote kinachotakiwa.
“Sisi ni wapenzi wa soka, hata soka hili la watu wenye ulemavu tunalipenda na kulishabikia. Baada ya kukaa na viongozi hawa kuna kiasi kikubwa cha fedha kinahitajika.
“Mnajua shughuli ya kuandaa mashindano ya Afrika, Serikali imechangia kwa pale imeona inaweza na sasa wadau wengine wanakaribishwa kwa ajili ya kuchangia kufanikisha mashindano haya,” amesema Bwire.
Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa timu ya soka ya watu wenye ulemavu (Tembo Wariors), Salvatory Edward, ametaja kikosi cha wachezaji 14 watakaongia kambini kujiandaa na mashindano hayo.