27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

HESLB, TASAF wajipanga kuwezesha kaya maskini

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, ameitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha Watanzania wahitaji na sifa za kujiunga na elimu ya juu wanawezeshwa.

Akizungumza katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Sebastian Inoshi, wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya taasisi hizo leo Jijini Dodoma, Dk. Akwilapo amesema upo umuhimu wa taasisi za Serikali kushirikiana katika kuwafikia wananchi na kutoa huduma.

Dk. Akwilapo amesema ni dhamira ya serikali kuhakikisha kuwa Watanzania wahitaji wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu wanapata mikopo na kutimiza ndoto zao, hivyo upo umuhimu mkubwa wa TASAF na HESLB kuhakikisha makubaliano haya yanatekelezwa kama inavyotarajiwa.

“Katika hili naomba niwape takwimu, mwaka 2019/2020, Serikali ilitoa sh bilioni 450 zilizowanufaisha wanafunzi 132,392, bajeti hii imeongezeka hadi kufikia sh bilioni 570 mwaka huu wa fedha wa 2021/2022 ambazo zitawanufaisha wanafunzi 160,000,amesema Dk. Akwilapo.

Pia Dk. Akwilapo ameitaka HESLB na TASAF ziongeze kasi ya kuunganishwa kwa mifumo ya TEHAMA ili kuwezesha utambuzi wa haraka na uhakika wa wanafunzi wanaotoka katika kaya masikini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaopata udahili katika taasisi za elimu ya juu nchini na ambao wapo katika mpango wa TASAF wanapata mikopo na kutimiza ndoto zao.

 “Makubaliano haya yatasaidia kuongeza ufanisi katika kubadilishana taarifa, hivyo na HESLB imejipanga kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu, wanafunzi wahitaji wahakikishe wanatimiza wajibu wao kwa kuomba mkopo kwa usahihi,” amesema Badru.

Naye Mkurugenzi Mtendaji TASAF, Ladislaus Mwamanga amesema taasisi hiyo itahakikisha inasimamia kwa umakini malengo ya  ushirikiano huo ili kuhakikisha wanafunzi wahitaji wanaotoka katika kaya maskini wanapata mikopo.

Makubaliano hayo yanaiwezesha HESLB kama taasisi ya mikopo ya wanafunzi kupanga mikopo kwa wanafunzi wahitaji kutoka katika mpango wetu, tumejipanga kuhakikisha kuwa mifumo yetu kuwatambua kwa haraka wanafunzi wote ambao wanakidhi vigezo vya kupangiwa mikopo ya elimu ya juu,” amesema Mwamanga. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles