Na Sheila Katikula, Mwanza
MKUU wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Hassan Masala amesema atashirikiana na viongozi wa idara mbalimbali pamoja na wananchi ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili kwenye maeneo yao.
Masala amesema hayo katika mkitano wa hadhara kwenye kata ya Buswelu wilayani Ilemela jijini hapa na kusisitiza kila kiongozi anawajibu wa kusimama kwenye nafasi yake na kutimiza majukumu kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na serikali.
Alisema lengo la ziara hiyo ya kuzingikia kata 19 za wilaya hiyo ni kutembelea miradi iliyopo na kuzungumza na wananchi ili kuweza kutambua changamoto zinazowakabili kwenye maeneo yao.
“Nimesikia mkizungumza kwa uchungu kuwa mnakabiliwa na changamoto ya umeme,maji kwenye maeneo yenu naomba tushirikiane kwa pamoja kwa sababu nyinyi ni sehemu ya kutatua nisingependa kusikia nikirudi tena baada ya miezi mitatu yanazungumziwa masuala haya.
Aidha amewataka viongozi kuacha kukaa ofisini na badala yake kutoka nje na kuzungumza na wananchi kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa kwani dhamira ya serikali ni kuhakikisha wanatekeleza ahadi zote kwa wananchi.
Meneja wa shirika la umeme Tanesco Nyakato, Mhandisi Edward Kweka amesema jitihada zinaendelea kufanyika kuhakikisha wananchi waliopo kwenye kata hiyo wanapata huduma hiyo kwa muda uliopangwa ili kuondoa kero ya umeme kwa wananchi ambayo wamekuwa wakiipigia kelele kwa muda mrefu.
Aidha Meneja wa kanda Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Mkoani Mwanza Kanda ya Nyakato na Kisesa, Mhandisi Josephat Ilunde amesema ifikapo Novemba 30 mwaka huu mradi wa maji uliopo kata ya Buswelu utakamilika na kupunguza changamoto hiyo kwa wananchi