Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema utaanza kujisafisha wenyewe kabla Rais Dk. John Magufuli hajakabidhiwa uenyekiti wa chama hicho.
Kauli hiyo, ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Hamasa, Sera, Utafiti na Mawasiliano wa umoja huo, Egla Mamoto, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema umoja huo, unapongeza hatua zilizochukuliwa na Rais Dk. Magufuli ndani ya siku 100 za uongozi wake.
“Tutajisafisha kabla Rais Dk. Magufuli hajakabidhiwa uenyekiti wa chama, kwa sababu bado kuna makandokando… kuna wasaliti ambao walitusaliti wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana, lazima tuwaondoe,” alisema.
Alisema watajisafisha ili kurudisha uadilifu ndani ya chama, wakati ambao wanajipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
“Tunajipanga kwa uchaguzi ujao, tuna kila sababu ya kuhakikisha tunaondoa wasaliti ili wasije wakatuangusha huko mbeleni,” alisema.
Akizungumzia juu ya vyama vilivyojitoa katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar unaotarajiwa kurudiwa Machi 20, alisema vyama hivyo vimejiua kidemokrasia.
“Wamejiua wenyewe na wanachama wao, CCM tutashiriki uchaguzi huu kwa sababu ni halali na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ipo huru kama ambavyo Rais amesema,” alisema.