Na Yohana Paul, Geita
VIJANA ni nguvu kazi ya taifa, hivyo ndivyo iilivyo, na ili nguvu kazi hiyo izae matunda ni lazima iwe yenye uwezo na utimamu wa akili na afya kwani ndiyo vigezo muhimu vinavyomwezesha mtu yeyote kufikia adhima ya uzalishaji mali ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.
Mbali na umuhimu wake, bado imekuwepo changamoto kubwa kwa vijana juu ya ufahamu wa elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango hali inayohatarisha mstakabari wa vijana wengi nchini kutokana na kuathirika afya ya mwili na akili pale wanapopata magonjwa ya zinaa, mimba za utotoni na mimba zisizotarajiwa.
Kwa kuliona hilo serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imeendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa makundi tofauti ndani ya jamii ikiwemo vijana, wajawazito, viongozi na wanandoa.
Kundi la vijana limeonekana kuwekewa mkazo zaidi kwani linatajwa kuathiriwa zaidi na changamoto zitokanazo na kutozingatia elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwani takwimu zinaonyesha asilimia 43 ya watu wote wanaoishi na virusi vya ukimwi ni vijana, miongoni mwao asilimia 80 wakiwa ni vijana wa kike, na hivyo wapo kwenye hatari kubwa sana ya ustawi wa maisha yao.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Geita
Akizungumzia hali na mwenendo wa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana mkoani Geita, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoani hapa, Last Lingson anasema elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ni muhimu kwa kuwa inagusa moja kwa moja mstakabari wa maisha na usalama wao.
Anasema, semina na warsha za elimu ya uzazi kwa vijana mkoani hapa zitasaidia sana kuwafanya vijana wakae kwenye nafasi ya kufahamu na kujitambua juu ya mabadiliko ya miili yao na kutambua hatua zipi za kufuaa ili wapate kuwa salama na wasiingie katika mianya inayoweza kuathiri ndoto zao
“Tunafahamu vijana wanaopevuka wanapokuwa kwenye hatua za ukuaji kuna wakati miili yao inaongozwa na hisia na matamanio, hivyo wakiwa na ufahamu juu ya afya ya uzazi itawasaidia vijana wote wa kike na wa kiume kukaa kwenye ufahamu wa tahadhari nini cha kufanya wanapofikia hatua hiyo.
“Hiyo itasaidia kuepusha mimba za utotoni ambazo huharibu ndoto za binti wengi na kupunguza maambukizi ya magonjwa ya zinaa kwa sababu afya ya uzazi inagusa moja kwa moja juu ya jinsi na jiinsia na tabia hatarishi zinazohusisha makundi rika na kwetu sisi kuwa na mpango wa afya ya uzazi kwa vijana ni jambo la muhimu sana ambalo tunatarajia litaleta mabadiriko makubwa sana,” anasema Lingson.
Anaongeza kuwa, kwa hali na mwenendo wa maisha ya sasa, njia sahihi ya kuwawezesha vijana kufikia malengo yao ni kuambatanisha elimu ya uzazi wa mpango na elimu ya mikopo na ujasiliamali kwani suala la changamoto za kiuchumi limekuwa na mchango mkubwa kupelekea mimba za utotoni hususani kwa vijana wa kike.
Anaeleza, kwa mkoa wa Geita vijana wengi wamejitahidi kufuata elimu ya uzazi lakini suala la umasikini limekuwa kikwazo na wanapopatia vishawishi vya kifedha wanajikuta wanajiingiza kwenye tamalaki ya magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa na kupelekea sintofahamu ya ndoto zao.
“Unapompatia kijana elimu ya afya ya uzazi na elimu ya mikopo ataweza kufanya ujasiliamali huku akitambua kuhusu mabadiliko ya kimwili na kiuzazi na atakuwa imara kwenye masuala ya kiuchumi hivyo kundi hili litakuwa imara na sisi kama jamii na taifa tutaweza kufikia mahala pazuri zaidi,” anasema
Anakiri kuwa imekuwepo changamoto kubwa kwa vijana wa kiume kushiriki semina na warsha za elimu ya afya ya uzazi na wengi hawazingatii lakini ni lazima watambue vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa na wanapaswa kuiwekea mkazo ili iweze kuwa na msaada kwa maendeleo yetu
Anasema, kwa vijana wa kiume kutozingatia na kutotambua umuhimu wa afya ya uzazi kwao imewafanya kukosa ufahamu wa mambo mengi na vijana wengi kuwa kwenye mazingira hatarishi ya kupata magonjwa ya zinaa na hata wengine kuwa wazazi katika umri mdogo na kukatisha ndoto zao na wenzi wao.
Anasema ili kuindokana na changamoto hiyo, serikali kwa kushirikiana na taasisi tofauti inaendelea kuhimiza vijana kuzingatia elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango inayotolewa na ni vyema wadau wote waunganishe nguvu kuwekeza katika elimu kwa vijana hasa zaidi vijana wa kiume kwa maana hao ndiyo wamekuwa washawishi wakubwa zaidi.
Anasema hadi sasa mkoa wa Geita unaendelea na mradi wa elimu hiyo kwenye halmashauri mbili ambazo ni Wilaya ya Geita na Chato, mradi unaofadhiriwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Nchini (TACAIDS) sambamba na Shirika la AMREF ambapo unawalenga zaidi vijana barehe na wazazi vijana kwa maana ya wale waliopata watoto wakiwa kwenye umri mdogo.
Mradi unalenga kuongeza ufahamu juu ya tabia hatarishi, na mfumo wa maisha unaoweza kuwaingiza kwenye hatari, vijana waliopo shuleni na wale walio nje ya shule ili kuwasaidia na kupata uelewa wa magonjwa ya zinaa, mimba za utotoni ambayo ni changamoto kubwa kwani vijana wengi hawana elimu hiyo.
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya mji wa Geita
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji ya Geita, Cathbert Byabato anasema hadi sasa wanaendelea na mradi wa TUPANGE PAMOJA ambao unawahusisha pia vijana, kulenga kuwawezesha kushiriki kwenye masuala ya uzazi ulio salama kiwasaidia watakapokuwa kwenye mahusiano waweze kutumia njia sahihi za kujikinga na mimba zisizotarajiwa na pengine anapopata ujauzito aweze kuhudhuria kliniki kufuatilia masuala yote ya kiafya.
Anaeleza kuwa, wamebaini vijana wakati mwingine wanapata aibu juu ya masuala ya afya ya uzazi hivyo wanapewa kipaumbele zaidi wanapokuja kwenye huduma za kiafya, na wanasisitiza kuwepo na sehemu maalumu ya vijana waweze kupokelewa na kupatiwa huduma zile stahiki kwa hali ya usiri na ufaragha kadri ya mahitaji yao.
“Mradi huu upo kwenye kata saba, ni mradi wa miaka mitano na tayari umeanza kutekelezwa kwenye kata ya Kalangalala, Kasamwa, Bulela, Ng’wangoko, Mtakuja, Nyankumbu, na Nyanguku ambapo kata hizi zipo katika mradi moja kwa moja lakini halmashauri kama idara ya afya imejipanga kuzifikia kata zote 15 ndani ya halmashauri ya mji wa Geita.
“Tunaendelea kusisitiza vijana ambao wapo tayari kupata mimba katika umri unaoruhusiwa basi waendelee kuzingatia njia bora ambazo zimeidhinishwa kwani idara ya afya inasisitiza angalau kuanzia umri wa miaka 21 ndiyo umri sahihi wa kupata mimba bila matatizo.
“Kwa sababu umri wa miaka 18 ni umri ambao bado mtu anakuwa katika kipindi cha kumalizia masomo yake kwa hiyo ni vizuri wanapoanza msuala ya familia wawe na uwezo wa kustahimili maana tunaamini wataweza kumudu malezi ya watoto na kukidhi mahitaji yao,” anasisitiza.
Anakiri kwamba uwepo wa mgodi mkoani hapa umesababisha vijana wengi walio katika umri barehe kuanzia miaka 15-24 wanaokuja kufanya shughuli za kiuchumi na baadaye kujiingiza kwenye mahusiano na kupata mimba zisizotarajiwa ingawa kwa takwimu zilizopo wengi walio na umri kuanzia miaka 18 ndio wanaopata mimba kwa idadi kubwa zaidi.
Byabato anawakumbusha vijana kuzingatia elimu ya uzazi wa mpango kwa kuwa jamii inahitaji maendeleo, na maendeleo yanatokana na maandalizi na mahusiano salama hivyo wasijiingize kwenye mahusiano pasipo kujiandaa kumudu chagamoto za kifamilia na malezi bora ya mtoto.
Afisa Maendeleo Vijana Halamshauri ya Mji wa Geita
Naye AfisaMaendeleo Vijana Halmashaurii ya mji wa Geita, Zengo Pole anasema ni ukweli ulio wazi kijana ili afikie malengo yakeni lazima aangalie suala la afya ya uzazi ili kuhakikisha anajilinda na kupanga na pale anapotaka kuoa au kuolewa ajaribu kujiwekea malengo yake juu ya idadi ya watoto anaoweza kuwamudu katika malezi.
“Elimu hii itawasaidia vijana kujitathimini uwezo wao, namna ya kuweza kuhimili kulea familia ingawa tunaamini watoto ndiyo nguvu kazi ndani ya familia, lakini ni lazima kuwe na mipango kwamba wanazaa watoto wangapi wanawamudu, ili kuondoa changamoto za kuzaa watoto kiholela na kuongeza idadi kubwa ya watoto wa mitaani,” anasisitiza.
Zengo anaeleza kuwa kwa siku za hivi karibuni imekuwepo ongezeko la watoto wa mitaani kutokana na watu wengi ikiwemo vijana kuzaa bila malengo na kuwaacha watoto waende wanakokujua jambo ambalo limefifisha ndoto za watoto hivyo ni lazima wajifunze kuweka mipango ya kuzaaa kulinda, kutunza na kuhudumia watoto badala ya kutelekeza.
Mtazamo wa Vijana.
Michael Mabula (24) mkazi wa mtaa wa Nyankumbu, kata ya Nyankumbu wilayani geita mkoani hapa anakiri kuwa kupata watoto wengi imekuwa ni moja yakikwazo kwake kufikia malengo yake kwani amekuwa akitumia pesa nyingi kuhudumia watoto hasa wanapougua ambapo kwa sasa ameamua kufuata misingi ya uzazi wa mpango na kusimama kwa muda kuzaa.
Rose Mapalala (23) makazi wa mtaa Shilabela kata ya Buhalahala anasema ni kweli aliwahi kupata mtoto wa kwanza akiwa na miaka 18 tu lakini baada ya kupatiwa ufahamu wa elimu ya uzazi aliamua kutumia uzazi wa mpango asiweze kupata ujauzito mwingine ili aendelee na shughuli za ujasiliamali wa kuuza chakula na imekuwa na msaada mkubwa kwake ikizingati wa kuwa baba wa mtoto amekuwa hashiriki kutoa matunzo kwa mtoto.