29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

WHC yatakiwa kujenga nyumba za gharama nafuu kwa watumishi wa umma

Na Faraja Masinde, Dar es Salaam

Serikali imeitaka Kampuni ya Nyumba ya Watumishi (WHC) kuhakikisha kuwa inajenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya watuishi wa kada ya chini wakiwamo makalani na watu wengine.

Wito huo umetolewa Jumatatu Juni 28, 2021 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa alipotembelea miradi ya WHC iliyoko Kigamboni, Magomeni na Bunju.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa akizungumza na watumishi wa Watumishi Housing Company (WHC) (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la Gezaulole Kigamboni na Magomeni jijini Dar es Salaam.

Mchengelwa ameitaka WHC kujenga nyumba ambazo zitaweza kuwasaidia watumishi wote wa umma ili kuweza kupunguza pengo la nyumba milioni tatu ambazo zinahitajika kwa ajili ya watumishi.

“Pamoja na kutekeleza miradi yenu vizuri na kwa ufanisi lakini niwakumbushe tu kwamba mnatakiwa kuwa wabunifu kwa kuangalia ni kwa namna gani katika kipindi hiki cha miaka minne na iliyobaki kufikia 2025 na 2030 mnakamlisha changamoto ya makazi kwa watumishi wa umma kwa kada zote.

“Hivyo, niwatake Watumishi Housing wale wanaohusika na eneo la ubunifu wawe wabunifu zaidi, kuona ni namna gani tunaweza kutafuta fedha za kuhakikisha tunatatua kero za watumishi wa umma hasa katika maeneo ambayo yanawatumishi wengi wa umma kama Dodoma makao makuu ya nchi ambapo kuna watumishi wengi wa umma ambao hawana mahali pa kukaa na hivyo wanalazimika kupangta kwenye nyumba binafsi hatua inayoongeza mzigo mkubwa kwao,” amesema Mchengerwa.

Amesema lengo la serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu ni kuona kufikia mwaka 2030 kero hiyo ya ukosefu wa nyumba kwa watumishi wa umma iwe imeondoka na hivyo kuwapa kazi WHC kushughulikia ndoto hiyo.

Mbali na hilo pia ameitaka WHC kutojiweka kibiashara zaidi badala yake kuona namna ya kuwasaidia zaidi watumishi wa umma katika kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumua yao wakiwa kwenye makazi bora.

“Noaomba mjipange vizuri, pamoja na kwamba mnajenga nyumba nzuri lakini muangalie namna ya kupunguza gharama za nyumba ili kumsaidia mtumishi wa kawaida kuweza kumudu gharama za nyumba. Hivyo hakikisheni kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na maeneo mingine yanayokua kujenga nyumba za kutosha na za gharama nafuu,” amesema Mchengerwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa (WHC), Dk. Fred Msemwa amesema ofisi yake itatekeleza maelekezo ya waziri kwa kuongeza ubunifu ili kujenga nyumba za gharama nafuu kwa watumishi kwenye majiji na maeneo yenye uhaba wa nyumba hususani vijijini na kwenye maeneo yenye huduma za shule na afya.

Moja ya miradi ya Watumishi Housing iliyoko KIgamboni Gezaulole jijini Dar es Salaam.

Dk. Msemwa ameahidi kuwa, ofisi yake itaendelea kubuni miradi itakayowahakikishia Watumishi wa Umma pamoja na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu kwa kuzingatia kipato chao.

Aidha, amemshukuru Mchengerwa kwa kuipongeza ofisi yake kwa ubunifu wa miradi ya nyumba ambazo zimewawezesha Watumishi wa Umma katika maeneo yenye miradi ya nyumba za Watumishi Housing kupata nyumba za kupanga na kuishi.

Awali, Dk. Msemwa wakati akimkaribisha Waziri Mchengelwa, alisema kuwa WHC inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo udogo wa mtaji, uhaba wa viwanja vya kutekeleza mitaji kila miji, upatikanaji wa mikopo sanjari na miundombinu ya maji na umeme.   

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles