25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi wanachama Simba utata mtupu

Ismail Aden Rage
Ismail Aden Rage

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

KESI iliyofunguliwa na wanachama wa Simba kuomba zuio la Uchaguzi Mkuu, imetawaliwa na utata mtupu baada ya mwanachama mmoja kuibuka na kuomba kuingia katika kesi kwa madai kwamba kuna mchezo mchafu ndani yake.

Mwanachama huyo, Shaaban Omari, anataka kuieleza mahakama mchezo mchafu uliopo katika kesi hiyo na kwamba ni vigumu kupata zuio bila kuwepo kwa kesi ya msingi mahakamani.

Utata huo ulionekana jana wakati maombi hayo ya zuio yalipotakiwa kusikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji, Augustine Mwarija.

Maombi ya zuio yalikwama baada ya mahakama kubaini kwamba, Rais wa Simba, Ismail Aden Rage hakuwepo mahakamani japo Wakili wa wadai, Revocatus Kuuli kudai kwamba alipokea hati ya kuitwa.

“Mheshimiwa Jaji tunaomba tuendelee kusikilizwa, tuko tayari,” alidai Kuuli.

“Rais wa Simba alipelekewa hati ya kuitwa mahakamani na kama alipelekewa uthibitisho uko wapi? Alihoji Jaji Mwarija.

Wakili Kuuli aliomba shauri liahirishwe ili waweze kuleta uthibitisho au Rage afike mahakamani. Jaji Mwarija aliamuru maombi hayo yasikilizwe leo na Rage afike mahakamani.

Wakati wanachama hao wakiomba zuio ndipo mwanachama huyo, Shaabani Omari akiwakilishwa na Wakili Jerome Msemwa na kuwasilisha maombi ya kuingia katika kesi kwa kujitegemea ili kuieleza mahakama mchezo mchafu unaoendelea ndani ya maombi ya zuio.

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu maombi hayo yaliyowasilishwa, Wakili Msemwa alidai kwamba tayari kuna maombi ya mteja wake mahakamani na aliamua kufanya hivyo baada ya kuona kuna mchezo mchafu.

“Tumewasilisha maombi namba 302/2004, mteja wangu anataka kuieleza mahakama kinachoendelea, wanachama wa Simba wamewasilisha maombi bila ya kuwepo kwa kesi ya msingi, zuio litatolewaje bila kuwepo kwa kesi ya msingi, kinachotangulia mahakamani ni kesi ya msingi.

“Wagombea hawakuhusishwa katika kesi, wadai wamewasilisha maombi ya zuio bila kuambatanisha Katiba ya Simba, sisi tumeambatanisha Katiba ya Simba katika maombi ya kujiunga, tunataka Jaji aone kilichomo ndani yake.

“Katika Katiba ya Simba, Ibara ya 55 inasema kwamba hairuhusiwi kutafuta msaada katika mahakama za kawaida za sheria.  Uamuzi wa mwisho uliochukuliwa na vyombo vya Simba Sports Club, maamuzi ya aina hiyo hayana budi kuwasilishwa katika Mamlaka ya Baraza la Usuluhishi. Ukiukwaji wa kanuni hii utasababisha kufukuzwa kutoka Simba Sports Club,” alidai Msemwa akinukuu ibara hiyo.

Msemwa alidai katiba hiyo inatamka kwamba rufaa inatakiwa kwenda TFF kisha inakwenda FIFA, lakini kufikisha suala hilo mahakamani ni kwenda kinyume na Katiba ya Simba.

Maombi ya Shaabani ni dhidi ya Josephat Waryoba, Said Monero, Hassan Hassan, Rais wa Simba na Bodi ya Wadhamini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles