Mdhamini akiri hali tete Simba

0
1265
mashabiki wa Simba wakifurahia mchezo
mashabiki wa Simba wakifurahia mchezo

Na Abducado Emmanuel, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Baraza la Wadhamini la Simba SC, Hamisi Kilomoni, amekiri kuwa kwa sasa hali ni tete kwenye klabu hiyo, baada ya kukosa umoja miongoni mwa wanachama, huku akidai suala hilo linahatarisha umoja wa baadaye ndani ya Simba.

Akizungumza na MTANZANIA jana alipokuwa akitoka kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kusikiliza kesi iliyofunguliwa na wanachama wa timu kupinga uchaguzi wa timu hiyo, Kilomoni alisema juhudi za makusudi zinatakiwa kufanywa haraka kumaliza hali hiyo ya hatari.

“Nimekuja mahakamani kusikiliza kesi ya wanachama ambayo mimi ni mmoja wa washtakiwa. Sijapendezwa na hali inayoendelea hivi sasa Simba kwa wanachama kuwa na makundi, kuna kazi ya ziada na ya haraka inatakiwa kufanyika ili kurudisha umoja huo kwani unahatarisha amani ndani ya Simba.”

“Baada ya kesho (leo) kumalizika kwa kesi hiyo, nitatoa tamko langu nikiwa kama mdhamini mwenye mali zote za klabu, hali ni tete kwa kweli tukiliachia hili litakuja kuimaliza klabu baadaye,” alisema Kilomoni.

Katika hatua nyingine alisema jana alishindwa kuongea chochote mahakamani baada ya kesi hiyo kuahirishwa, huku akieleza kuwa leo hii anaweza kuzungumza kuhusiana na madai waliyoshtakiwa na wanachama hao wa Simba.

Uchaguzi Mkuu wa Simba umepangwa kufanyika keshokutwa kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here