NA HADIJA OMARY, LINDI
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telak, leo Agost 23 amepokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam Amos Makala na unatarajia kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali mkoani hapa.
Makabidiano ya mwenge huo yamefanyika katika kijiji cha Malendego, wilayani Kilwa yakihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Mkoa na Wilaya pamoja na wananchi wa maeneo hayo na maeneo jirani.
Akipokea Mwenge huo Zainabu, amesema utakimbizwa katika wilaya tano za mkoa huo kwa umbali wa kilometa 815.8 na utatembelea, utazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo 42 yenye thamani ya sh. 12.7 bilioni.
Zainab amesema kati ya miradi hiyo 42, miradi 10 itawekwa mawe ya msingi,14 itazinduliwa na miradi 15 itakaguliwa ambapo mchango wa Serikali Kuu ikiwa ni sh. 9 .04 bilioni, Halmashauri imechangia bilioni 1.66, nguvu za wananchi bilioni 1.6 na wadau wa maendeleo ni milioni 918.6
Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Luten Mwambashi, amewatahadharisha viongozi wa mkoa na wilaya kuwa na nyaraka zote muhimu katika miradi husika ambayo itatembelewa na Mwenge huo ili waweze kuzipitia kwa kina na kujiridhisha.
“Naomba niwakumbushe viongozi wangu wa Mkoa wa Lindi katika miradi yote tutakayotembelea huko wilayani kwenu naomba nyaraka zote zinazohusika ziwepo na tuzipate asubuhi mapema kabla hatujaanza kutembelea miradi yenyewe hii itatupa sisi urahisi wa kuzipitia taarifa mapema,” amesema Mwambashi.
Hata hivyo Mwambashi amesema kutokana na uwepo wa ugonjwa wa uviko 19 watu wote watakaoshiriki kwenye mbio hizo za mwenge wanapaswa kuendelea kuchukuwa taadhari juu ya ugonjwa huo ikiwa pamoja na kuvaa barakoa, kunawa maji tiririka na kutumia vitakasa mikono mara kwa mara.