NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema kurejea kikosini kwa kiungo, Haruna Niyonzima, ni jambo la furaha kwani timu hiyo inahitaji mchezaji wa aina yake mwenye uwezo wa kuwatetemesha wapinzani.
Ijumaa ya wiki iliyopita uongozi wa klabu ya Yanga ulimaliza tofauti zilizokuwepo kati yake na Niyonzima na juzi aliingia rasmi uwanjani kucheza dhidi ya Friends Rangers katika mchezo wa Kombe la FA.
Katika mchezo huo uliopigwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga walishinda mabao 3-0 na kufanikiwa kutinga hatua ya 16 ya Kombe la FA ili kuwania tiketi ya kufuzu kucheza Kombe la Shirikisho mwaka 2017.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Pluijm alisema si kwamba katika kikosi chake hakuna wachezaji wazuri bali uwezo na sifa alizonazo kiungo huyo ni muhimu kwa timu hiyo.
Akizungumzia mchezo wa juzi, Pluijm alisema hakupata tabu ya kuwafunga wapinzani wao kwa kuwa anawafahamu vizuri kwani walishakutana mara mbili kwenye mechi za kirafiki.
“Niliwasoma vizuri kwenye mechi mbili tulizocheza, hivyo ilikuwa ni kazi rahisi kuwakabili na kuhakikisha tunapata mabao ya mapema kwani ndiyo njia inayoweza kuwatoa mchezoni na kutupa nafasi ya kufunga zaidi,” alisema.
Alisema nyota sita wa kikosi hicho walikuwa wakisumbuliwa na majeraha, lakini aliowapa nafasi walionyesha uwezo mkubwa na kufanikiwa kuipa timu ushindi ingawa wangeweza kufunga mabao mengi zaidi.