30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

500,000 wampinga Trump

U.S. Republican presidential candidate Donald Trump waves during a campaign rally in Cedar Rapids

WASHINGTON, Marekani

TAIFA la Marekani, ambalo linatajwa kuwa ‘baba wa demokrasia’, limejaribiwa baada ya siku mbili mfululizo kushuhudiwa maandamano makubwa ambayo sasa yamezaa ghasia, wakipinga ushindi wa Rais mteule wa nchi hiyo, Donald Trump.

Pamoja na maandamano hayo, hadi kufikia jana watu 500,000 walikuwa wamesaini azimio la kutaka ufutwe mfumo wa kura za wajumbe (Electoral College) ambao unatoa nafasi ya kuamua nani awe mshindi wa kiti cha urais.

Idadi hiyo ya watu waliosaini azimio hilo inaelezwa kuwa ni zaidi ya nusu ya saini zinazohitajika ili liweze kufikishwa kwenye vyombo vya maamuzi.

Saini za azimio hilo zilizoanza kukusanywa Jumatano baada ya Trump kutangazwa mshindi, linadai kuwa rais huyo mteule hafai kuitumikia Marekani, kwa sababu ni mwongo, mnyanyasaji na ana historia ya kunyanyasa wanawake kingono na hana uzoefu wa kiuongozi na hivyo kuhatarisha umma wa Marekani.

Trump alitangazwa mshindi wa kiti  hicho  Novemba 8, mwaka huu, baada ya kupata kura za wajumbe 276 dhidi ya 218 za Hillary Clinton wa chama cha Democrat, ushindi ambao unahitimisha utawala wa miaka nane wa chama hicho kilichoingia mwaka 2008 kupitia Barrack Obama.

Kwa mujibu wa mabadiliko ya kwanza ya Katiba ya Marekani, yanatambua haki ya watu kutoa dukuduku, mfano kupitia maazimio kama hayo, lakini haibadili matokeo yanayotambuliwa na mfumo.

Pamoja na hayo, kwa siku ya pili jana umati wa waandamanaji wenye hasira uliingia mitaani katika maeneo mbalimbali ya Marekani, huku vikiripotiwa vitendo vya wizi, kuchoma moto bendera ya nchi hiyo, magari na kuvunja maduka.

Maandamano hayo ambayo yalianzia Jimbo la California, dakika chache tu baada ya Trump kutangazwa mshindi, jana yalifika Portland, Oregon na waandamanaji walisikika wakipaza sauti “si rais wetu, F*** Donald Trump”.

Maandamano hayo yanachagizwa na hoja za kibaguzi ambazo Trump alikaririwa kwa nyakati tofauti kabla na baada ya kampeni za kuwania urais wa nchi hiyo kuanza.

Magenge ya kihalifu yanadaiwa kutumia mwanya wa maandamano hayo kubomoa maduka na kupora mali za wananchi.

Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, jana liliripoti kuwa maandamano hayo yametawaliwa na kundi kubwa la vijana wanaodai kwamba uongozi wa Trump utazua migawanyiko kwa misingi ya rangi na jinsia.

Wakati huo huo, Polisi wa Mji wa Portland wamesema,  wamekabiliana na magenge ya waporaji pamoja na kundi jingine la watu lililokuwa linawashambulia wenzao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Polisi wa Portland, Oregon, maandamano hayo yanatakiwa kuchukuliwa kama ghasia kutokana na waandamanaji kuvunja majengo na maduka.

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba, baadhi ya waandamanaji wamebeba mabango, magongo na mawe kuharibu mali za watu.

Ingawa hakujaripotiwa kifo tangu kuanza kwa maandamano hayo, lakini waandamanaji wamefunga baadhi ya barabara muhimu zinazounganisha viunga mbalimbali vya miji mikubwa nchini humo.

BBC imeripoti kuwa, mjini Philadelphia, umati mkubwa wa watu ulikusanyika nje ya ukumbi wa baraza la jiji na kuimba nyimbo za “Si Rais Wetu,  Ifanye Marekani iwe salama kwa wote”.

Taarifa iliyotolewa na Polisi wa mji wa Baltimore inatanabahisha kuwa waandamanaji 600 walizuia magari kupita katika barabara kuu inayoingia katika mji huo.

Wakati hayo yakijiri, Rais huyo mteule juzi alikutana na Rais Barack Obama Ikulu, kwa ajili ya shughuli ya mpito ya kupokezana madaraka ambayo itachukua wiki 10 hadi kuapishwa kwake.

Baada ya mkutano wao wa faragha uliofanyika Ikulu ya Marekani (White House), Trump alisema mkutano wao ulikuwa wa kufana na akaahidi kuwa tayari kubadilisha mambo mengi aliyoyafanya Rais Obama alipokuwa madarakani.

Miongoni mwa hayo ni mpango wa Afya uitwao Obamacare, sheria ya bima ya taifa iliyowawezesha Wamarekani wengi zaidi kupata matibabu.

Kuhusu maandamano ya kumpinga yanayoendelea, Trump aliandika kupitia mtandao wa Twitter  akisema; “ni uchaguzi wa  urais wa wazi tu na mafanikio. Sasa wataalamu wa maandamano ambao wamechochewa na vyombo vya habari, wanaandamana. Si haki kabisa!”

Kabla ya kufanya mkutano wa faragha na Trump juzi, Rais Barack Obama  aliwaomba  Wamarekani kuwa watulivu na kumpa ushirikiano rais huyo mteule.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, Obama na mkewe, Michelle, walishiriki kwa nguvu kujaribu kuzuia ushindi wa Trump, wakisema hafai kuongoza.

Wakati fulani Obama alisema Trump hafai hata kuwa muuza duka.

Hata hivyo, baada ya matokeo kutangazwa, Rais huyo anayemaliza muda wake, amewahimiza Wamarekani wote kuyakubali.

“Sasa tunatafuta ufanisi wake katika kuunganisha na kuongoza nchi hii. Tumpe ushirikiano,” alisema Obama.

Wakati  Rais Obama akihimiza umoja baada ya uchaguzi,  aliyekuwa mpinzani wa Trump katika kinyang’anyiro hicho, Hillary Clinton, naye aliwaambia wafuasi wake wampe nafasi Trump aongoze, huku naye akimuahidi ushirikiano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles