26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Ndalichako amekosea sifa ya kuchukua Shahada

Waziri  wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako

WASOMI, wadau wa elimu na wananchi wa kawaida wamekosoa tamko la Waziri  wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, wakisema kwamba halijafanyiwa utafiti na halitekelezeki kisheria.

Kwamba mwishoni mwa wiki, akiwa kwenye mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Ndalichako, alisema kuanzia mwakani mwanafunzi yeyote hatajiunga na masomo ya Shahada bila kupitia kidato cha sita.

Kwamba mfumo wa elimu huria umechangia kuzalisha wasomi butu kwa kupokea wanafunzi dhaifu kitaaluma.

Wakizungumzia tamko hilo  katika maeneo mbalimbali nchini, baadhi ya wasomi wanasema kabla ya waziri kuanza kutoa amri na matamko, alitakiwa kufanya utafiti kujiridhisha juu ya agizo lake hilo.

Kwamba Profesa Ndalichako hajasema ametoa wapi ujasiri wa tamko lake hilo, kama ni kwa utafiti aliofanya yeye au hata kukasimu taasisi kwa niaba yake ili ifanye utafiti na kuja na majibu kuwa kidato cha sita ndicho kiwango bora cha kumpitisha mtu kusoma Shahada ya kwanza.

Kwamba tamko lake ni la kisiasa lisiloweza kutekelezwa kisheria.

Kwamba inabidi kwanza arekebishe sheria kabla ya kutoa tamko la kurekebisha mfumo wa elimu vinginevyo ataharibu kuliko waliomtangulia.

Kwamba pamoja na lengo zuri la kurekebisha mfumo wa elimu, badala ya kuanza na amri na matamko, Serikali inatakiwa kurekebisha kasoro zilizopo hatua kwa hatua.

Kwamba upo ushahidi wa kuwapo kwa wasomi wengi wakiwamo wale wanaofundisha vyuo mbalimbali nchini, vikiwamo vyuo vikuu, waliopitia ngazi ya chini kabisa ya cheti na sasa ni maprofesa na waliwafundisha hawa wanaobeza ngazi hizo.

Kwamba wapo majaji ambao walianza kazi ya ukarani mahakamani, wakajiendeleza kwa kusoma Chuo cha Mahakama Lushoto ngazi ya cheti, sasa ni madaktari na maprofesa wa sheria tunawategemea.

Kwamba haieleweki kama alichokisema Waziri Ndalichako ni tamko na uamuzi wa Serikali, kwani suala hilo haliko kwenye sera ya elimu, na si njia sahihi ya kuboresha elimu nchini mbali na kuwa kinyume cha utaratibu wa elimu kote duniani.

Kwamba mfumo uliopo unakubalika duniani kote na ndio ulioleta msemo wa ‘elimu haina mwisho’.

Kwamba Profesa Ndalichako haeleweki kwanini ameona diploma kwenda chuo kikuu ndiyo tatizo wakati watu wote wana haki ya kujengewa mazingira ya kujiendeleza kielimu.

Kwamba kuna watu wengi walikuwa na elimu ya ualimu ‘Grade’ C wa shule ya msingi lakini wamejiendeleza hadi wamekuwa maprofesa; na wengine wengi na waliopitia mfumo wa Cheti-Stashahada wanakuwa na uzoefu mkubwa kuliko wa kidato cha sita na wanafanya vizuri wakifika chuo kikuu.

Kwamba Serikali ikamilishe mchakato kwa kupeleka rasimu ya sheria mpya ya elimu bungeni, ili pawepo na Baraza la Taifa la Elimu, ambalo litakuwa na wawakilishi kutoka sekta ya umma, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na sekta binafsi,  ambayo itaandaa nyaraka (regulations) zote kabla hazijawekewa sahihi na kamishna wa elimu na pengine kutamkwa na waziri.

Tunasema Watanzania wameonyesha kukataa kwa hoja kuntu  maelekezo ya Profesa Ndalichako, hoja ambazo zimejikita kwenye sheria.

Tunamsihi sana Profesa Ndalichako akubali hoja hizi kwa manufaa ya Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles