Na DERICK MILTON – MASWA
WATU 18 wilayani Maswa, mkoani Simiyu waliotuhumiwa kwa makosa ya kuwapa mimba wanafunzi na ndoa za utotoni wamehukumiwa kwenda jela baada ya kutiwa hatiani.
Watu hao walipewa adhabu hiyo katika kipindi cha kuanzia Januari, mwaka jana hadi Mei, mwaka huu na kwa mwaka jana pekee walihukumiwa watu 13 na mwaka huu wamehukumiwa watano.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Seif Shekalage, wakati wa kikao cha tathmini ya kampeni ya Tokomeza Mimba na Ndoa za Utotoni, iliyoanzishwa na ofisi yake kwa kushirikiana na Shirika la World Vision Tanzania.
Shekalage alisema tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo mwaka jana, wamepata mafanikio makubwa, ikiwamo watuhumiwa kufungwa jela kuliko ilivyokuwa zamani pamoja na kesi nyingi kufikishwa mahakamani.
“Watu 18 kufungwa ndani ya mwaka mmoja na miezi mitano ni mafanikio makubwa, bila ya kampeni hii tusingefika hapa, tulipeana majukumu kila mdau atimize wajibu wake, ndiyo maana tumefikia hapa.
“Toka nimefika hapa hatujawahi kupata mafanikio kama haya, na kesi nyingi zilikuwa haziripotiwi, mtoto anapewa mimba wazazi na mtuhumiwa wanamalizana, lakini kupitia kampeni hii watu wameelimishwa,” alisema.
Alisema licha ya kuwapo kwa mafanikio hayo, bado viongozi wa kisiasa wamekuwa kikwazo kikubwa kwa baadhi ya kesi kutokana na kuingilia kati, ikiwamo wengine kutounga mkono kampeni hiyo.
Alisema viongozi wa Serikali za Vijiji, Vitongoji na madiwani hawaungi mkono kampeni hiyo kwa maelezo kuwa inawaharibia katika harakati zao za kutafuta kura au kulinda wapiga kura wao.
“Kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa bila ya kujali wanatoka chama gani niliagiza wakamatwe na kuwekwa ndani baada ya kutaka kuharibu baadhi ya kesi, na hili ni tatizo kubwa, lakini lazima tupambane nalo katika kunusuru maisha ya watoto hawa,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa World Vision Kanda ya Nzega, John Massenza, alisema bado nguvu kubwa inahitajika kwa wadau wote kushirikiana katika kutokomeza kabisa tatizo hilo.
Massenza alisema kupitia kampeni hiyo, wamekuwa wakitoa elimu kwa wanafunzi, wazazi na viongozi mbalimbali juu ya kupiga vita mimba na ndoa za utotoni.
“Tuliamua kuanzisha kampeni hii ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kupiga vita ukatili wa kijinsia na Simiyu ni miongoni mwa maeneo ambayo yamekithiri kwa vitendo hivi, hivyo kama wadau, tuliona kuungana na jamii, Serikali katika kuhakikisha tunavikomesha,” alisema.
Naye Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa, Fredrick Lukuna, alisema wanasiasa wengi wamegeuza ndoa na mimba za utotoni kama mtaji na biashara kwao kutokana na kuhusika katika harakati zote.
Pia alisema wanasiasa wamekuwa kikwazo kikubwa katika utolewaji wa ushahidi mahakamani kutokana na kuwashawishi mashahidi kuharibu ushahidi au kutoweka kusikojulikana.