31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Thamani ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) yafikia trilioni 5.8/-

Na Frank Mvungi

– MAELEZO

THAMANI ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), imefikia Sh trilioni 5.8.

 Akizungumza katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Hosea Kashimba, amesema kuunganishwa kwa mifuko ya GEPF, LAPF, PSPF na PPF, kunatoa fursa ya kuimarisha zaidi sekta ya hifadhi ya jamii hali iliyochangia thamani ya mfuko mpya wa PSSSF kuendelea kukua hata katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake.

“Tumeshatumia zaidi ya trilioni moja kulipa mafao kwa wanachama wetu hali inayoonyesha kuwa mfuko upo katika hali nzuri, hivyo niwatoe hofu wanachama wetu kwani tumejipanga kuhakikisha tunawahudumia vizuri kwa mujibu wa sheria na kanuni za hifadhi ya jamii,” alisisitiza Kashimba.

Akifafanua, Kashimba amesema  wastaafu elfu kumi wameshalipwa mafao yao tangu kuanzishwa kwa mfuko huo na wachache ambao hawajalipwa ni wale ambao hawajahakiki taarifa zao kwa muda uliotolewa hivyo aliwataka kujitokeza na kuhakikiwa ili warejeshwe katika daftari la malipo.

“Ukishahakikiwa tunakurejesha kwenye daftari la malipo na utalipwa malipo yako yote ambayo hukuwa umelipwa hapo awali kabla ya kuhakikiwa hivyo niwatoe hofu wanachama wetu na kuwataka wajitokeze kuhakiki taarifa zao,” alisisitiza Kashimba.

Alieleza kuwa takribani wastaafu 113,000 wamehakikiwa kati ya wastaafu 124,000 waliotakiwa kuhakikiwa, hivyo kuwaomba wanachama wa mfuko huo nchini kuendelea kujitokeza kuhakikiwa kupitia ofisi za mikoani kwa kuwa huduma zinazotolewa makao makuu  zinatolewa pia mikoani.

Kashimba aliwataka wanachama wote kuhakikisha kuwa waajiri wanawasilisha michango yao kwa wakati ili kuepuka usumbufu wakati wa kustaafu.

Akizungumza kuhusu ujenzi wa uchumi wa viwanda, Kashimba amesema mfuko huo umejipanga kuendelea kutekeleza dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali kulingana na miongozo ya Serikali.

“Tumewekeza katika Kiwanda cha viatu Karanga Moshi kwa ubia na Jeshi la Magereza na tunatarajia kiwanda hiki kitatoa ajira elfu nne na kuzalisha jozi milioni 1.2 kwa mwaka, tunawekeza kwenye kiwanda cha kuchakata tangawizi kilichopo wilayani Same, Kiwanda cha nyama Morogoro na vingine kulingana na miongozo ya uwekezaji na maagizo ya Serikali,” alisisitiza Kashimba.

Aidha, alisema mitambo ya kuzalisha viatu katika kiwanda cha karanga inatarajiwa kuwasili nchini na kufungwa katika kiwanda hicho kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa mfuko huo, Victor Kikoti, amesema baadhi ya mafao yanayotolewa ni yale ya muda mfupi na muda mrefu lengo likiwa kuwawezesha wanachama wote kuishi maisha bora hata baada ya kustaafu.

“Wanachama wetu wataendelea kunufaika na huduma zetu na hata pale inapotokea bahati mbaya mwanachama wetu amefariki basi haki zake hazitapotea na zinalindwa kwa mujibu wa sheria ili ziwanufaishe warithi wake,” alisisitiza Kikoti.

Naye Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Gilbert Chale, amesema mfuko huo umejenga mifumo bora inayounganisha ofisi zote na makao makuu ya mfuko ili kuimarisha huduma na tija kwa wanachama.

Kuunganishwa kwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF, GEPF, LAPF na PSPF kumewezesha kuanza rasmi kwa mfuko mpya wa Hifadhi ya Jamii katika Utumishi wa Umma (PSSSF) mwaka 2018. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles