Na Ramadhan Libenanga, Morogoro
JESHI la Polisi mkoani Morogoro, linawashikilia watu 10 waliokamatwa msikitini wakiwa na vifaa mbalimbali, ikiwamo milipuko 30, sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na bendera nyeusi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonald Paul alisema tukio hilo lilitokea Aprili 14, mwaka huu saa 3.30 usiku katika Kitongoji cha Nyandero, Tarafa ya Kidadu wilayani Kilombero.
Kamanda Paul alisema watu hao walikamatwa katika Msikiti wa Suni uliopo Kidatu, ambapo mmoja kati ya watu hao ambaye anadaiwa kuwa mwenyeji wa kundi hilo, aliuawa na wananchi kwa kuchomwa moto.
Kamanda Paul alimtaja mtu huyo kuwa ni Hamad Makwendo Mkazi wa Manyasini Ruaha wilayani Kilombero.
Alisema siku ya tukio, polisi walipata taarifa za watu wanaojihusisha na uhalifu na kuanza kufuatilia tukio hilo na kwamba baada ya kufika eneo la tukio walikuta watu hao wameondoka.
“Askari wetu walipofika pale walikuta watuhumiwa wote wameondoka kwa kutumia usafiri wa bajaji mbili,”alisema Kamanda Paul.
Alisema wakati wakiendelea na ufutiliaji, walikutana na bajaji moja ikiwa na abiria mmoja ambapo walilazimika kuisimamisha.
Alisema baada ya kuisimamisha bajaji hiyo, mtu mmoja aliruka na kuanza kukimbia ndipo askari mwenye namba F.3323 Koplo Nasoro alianza kumkimbiza na alipomkaribia mtuhumiwa huyo alichomoa jambia na kumkata askari huyo shingoni.
Alisema askari mwingine mwenye namba E9245 Koplo Chomola ambaye alikuwa nyuma, alifanikiwa kumpiga risasi ya mguu mtuhumiwa huyo na kuanguka chini.
Alisema baada ya kuanguka, wananchi wa eneo hilo tayari walikuwa wamefika na kuanza kumshambulia na baadae kumchoma moto.
Hata hivyo, Kamanda Paul alisema iliwalazimu kuongeza askari wengine ili kuwasaka watu wengine ambapo walipata taarifa za uwepo wa watu msikitini humo.
Alisema polisi walipofika katika msikiti huo, waliomba viongozi wa msikiti kuwatoa watu wote waliokuwamo msikitini ili kuwabaini wahalifu kwa sababu wanatiliwa shaka.
Alisema waumini wote walitakiwa kutoka nje ya msikiti wakiwa na mabegi yao, ambapo polisi waliendesha ukaguzi na kufanikiwa kuwakamata watu kumi.
Kwa mujibu wa Kamanda Paul, vitu vilivyokutwa katika mabegi hayo ni pamoja na milipuko 30 na bendera nyeusi iliyoandikwa maneno ya Kiarabu na Kiswahili yenye maana ya Mungu Mmoja.
Vifaa vingine walivyokutwa navyo ni nyaya za umeme, majambia , bisibisi, vifaa vya kujikinga puani (maski), sare moja ya Jeshi la Wananchi na nyingine ambazo hazikujulikana kutoka nchi gani.
Vifaa vingine walivyokutwa navyo ni misumeno, spana ya kufungulia mabomba, madaftari na vitabu mbalimbali vikiwemo vya risiti.
Alisema mbali na vitu hivyo, marehemu alikutwa na risasi sita, kati ya hizo tano ni za Sub Machine Gun (SMG) na moja ni ya bunduki ya Mark IV.
Kamanda Paul alisema, askari aliyejeruhiwa alitokwa damu nyingi na alikimbizwa katika Hospitali ya Kiwanda cha Sukari cha Kilombero na hali yake inaendelea vizuri.