Ramadhan Hassan,Dodoma
Mbunge wa Bukoba Mjini,Wilfred Lwakatare (Chadema) amesema kutokana na mafuriko yanayotokea katika Mji huo maji yamesambaa kiasi cha kupelekea watu kutoka katika mtaa mmoja kwenda mwingine kwa kutumia mtumbwi.
Akiomba mwongozo bungeni leo Mei 28,Lwakatare amesema hali ni tete katika eneo la Bukoba kufuatia mvua ambazo zimeendelea kunyesha kuathiri wakazi wa maeneo hayo.
“Kufuatia mvua ambazo zimeendelea kunyesha hivi sasa kuna mafuriko makubwa sana katika Manispaa ya Bukoba ambapo mtu mmoja mbaye ni mtoto amefariki na nyumba zaidi ya 75 zimepata maafa makubwa.
“pia maji yale yamesambaa ndani ya mji kiasi cha kupelekea watu kutoka katika mtaa kwenda mtaa mwingine kutumia mtumbwi.
“Kwa hiyo naleta hoja Mheshimiwa Mwenyekiti kwamba unikubalie hoja hii ili iweze kujadiliwa kwa maslahi mapana ya watu wa Bukoba ili hali inayoendelea ambayo imewaweka katika wasiwasi na kufikiria labda ule Mji umelaaniwa kutokana na matukio ambayo yanaendelea kutokea,”amesema Lwakatare
Akijibu,mwongozo huo,Mwenyekiti wa Bunge,Najma Giga amesema : “Suala la Rwekatare hatuwezi kulijalidi kwa sababu suala la mvua linatokea maeneo mengi nchini ni jukumu la Serikali kulifanyia kazi jambo hilo.