29.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 30, 2024

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Simbachawene ampiga mfanyabiashara

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa zamani wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, ameingia matatani baada ya kudaiwa kumshambulia mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam, Kassim Abdallah (37) hadi kusababisha alazwe Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe (CCM), anadaiwa kutenda tukio hilo Jumatatu wiki hii eneo la Vingunguti, wilayani Ilala.

Abdallah ambaye ni dereva, hivi sasa amelazwa  Muhimbili akipatiwa matibabu ya majeraha. Aliumia kichwani na sehemu nyingine za mwili.

Akizungumza na MTANZANIA juzi, Abdallah aliyelazwa wodi namba 18 ya wagonjwa binafsi kwenye jengo la Sewahaji, alisema alikumbwa na mkasa huo Jumatatu usiku alipokuwa katika harakati za kwenda kuegesha gari ofisini kwao.

Dereva huyo alikuwa akitoka safarini Rwanda na alisema ‘yard’ yao iko jirani na baa ya Titanic mahali ambako tukio lilitokea.

“Ilikuwa saa 6 usiku, nilikuwa nakwenda kuegesha gari na yeye (Simbachawene) alikuwa ameegesha gari jirani na baa, nilisimama mbali kidogo nikamuwashia taa, alifungua mlango akatoka na kuniambia nitulie.

“Nilidhani labda atasogeza gari, alikuwa amekaa ananiangalia, nilimuwashia tena taa, lakini alitoka na kuanza kucheza,” alisema Abdallah.

Alisema baada ya kuona mbunge huyo hajasogeza gari, aliamua kuwaomba vijana wa bodaboda waliokuwa jirani na eneo hilo wasogeze pikipiki zao ili aweze kupita.

“Niliporudi nyuma nilimuona kwenye kioo cha pembeni anakuja, nilikaa usawa wa geti nikapiga honi mlinzi aje afungue.

“Wakati najiandaa kuingia ndani nikaona meneja wake amenifuata akawa anasema mkuu (Simbachawene) analalamika nimepita karibu na gari lake.

“Nikamwambia sijaligusa, ghafla nikaona Simbachawene amekuja na kundi la watu akiwamo mwanawe Daudi.

“Akaniambia mimi ni jeuri, nikamuuliza kwanini, akasema kwanini nipite karibu na gari lake, atanionyesha adabu… akanizaba kibao, watu wakinizuia nisifanye chochote, nikaona busara nitulie tu,” alisema.

Kwa mujibu wa Abdallah, pia alishambuliwa na watu aliodai kuwa ni walinzi wa baa hiyo na mtoto wa mbunge huyo.

“Daudi (mtoto wa Simbachawene) alining’ata mkono wa kushoto na wengine walikuwa wananipiga bakora na marungu mikononi na kichwani,” alisema.

Abdallah alisema vijana wa bodaboda waliokuwa jirani walishirikiana na utingo wake na kumsaidia akainuka kisha kumpeleka katika Kituo cha Polisi Buguruni.

Alisema alitoa taarifa katika kituo hicho kisha kupewa fomu ya matibabu (PF3) na RB namba 11587/2018 ya shambulio la kudhuru mwili ambayo MTANZANIA imefanikiwa kuiona.

Abdallah alisema bado anasikia maumivu makali mwilini, hasa sehemu za kichwani na mikononi.

Sehemu ya kichwani alikuwa na alama ya kipigo na mkono wa kushoto pia ulikuwa umevimba ukiwa na alama za fimbo.

SIMBACHAWENE

Akizungumza na MTANZANIA jana, Simbachawene alikiri kufahamu tukio hilo na kusisitiza kuwa hakuwapo wakati kijana huyo anapigwa.

“Ni kweli kulitokea tukio hilo siku ya tarehe 23, huyo kijana alipotoka na gari lake aliingia katika mazingira ambayo alikuwa na fujo.

“Na pale ni pembamba, akaingia na gari kama anapita kwenye barabara kubwa na kila mtu alihamaki, vijana wa bodaboda, wateja na mimi nilikuwa mmojawapo katika watu waliohamaki.

“Nilikuwa ndio naanza kuondoka, kosa lililotokea ni kwamba viongozi wa pale kwenye baa hawakuwa ‘active’ kama siku zote, kwamba mtu anapoleta fujo wanawahi kuripoti polisi.

“Wakati linatokea hilo mpaka anachapwa na walinzi mimi nilikuwa nimeshaondoka, kwahiyo sikujua kilichotokea nyuma. Mpaka kijana wangu alipokuja kukamatwa ndio nilipata taarifa ya kilichotokea jana yake,” alisema.

Alisema aliitwa kwenda kutoa maelezo polisi na alitii wito huo kwani tuhuma si kitu cha ajabu.

“Nilipigiwa na polisi, nimeenda nimetoa maelezo kwa sababu ni tuhuma na si kitu cha ajabu, kwahiyo taratibu za kisheria zimefuatwa, hivyo wanaendela kupeleleza,” alisema.

Hata hivyo, Simbachawene alisema wameanza mazungumzo ya kifamilia kwa sababu anafahamiana na kijana huyo na ndugu zake.

“Tuko pamoja geti hili na lile, ananifahamu lakini hata magari yangu yanaegeshwa kwenye ‘yard’ yao, tunaweza kuingia kwenye ligi isiyokuwa na sababu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles