26.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 7, 2021

Kituo cha biashara EAC kujengwa stendi ya Ubungo

Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAA

KITUO kikubwa cha biashara cha kimataifa kinatarajiwa kujengwa katika eneo la Stendi ya Mabasi ya Ubungo, ujenzi utakaoanza Januari mwakani na kuchukua miezi 18 kukamilika.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa Mauzo wa Kampuni ya East Africa Commercial & Logistics Center Tom Zhang, alisema kitakapokamilika kituo hicho kinatarajiwa kuwa namba moja kwa nchi za Afrika Mashariki.

Alisema kwa sasa tayari wana vituo viwili vya aina hiyo, cha kwanza kikiitwa Dragon Mall ambacho kipo nchini Dubai na kingine kikiitwa Yiwu City Mall nchini China.

“Kituo hiki kitakuwa maalumu kwa ajili ya kuingiza bidhaa kutoka nje na kuuza bidhaa kwenda nje. Kutakuwa karibu na kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya biashara za kimataifa.

“Hii ina maana kwamba kikishakamilika, hakutakuwa na sababu ya mfanyabiashara wa Tanzania kusafiri kwenda China au nje ya nchi kununua bidhaa na kuzileta nchini. Safari hizo zinagharimu muda mwingi na gharama kubwa ambazo sio za lazima.

“Kwahiyo hapa tutakuwa na ofisi za kampuni zote zinazozalisha bidhaa nje ya nchi na hata za ndani. Mfanyabiashara atachukua bidhaa kwa kuagiza moja kwa moja kiwandani akiwa hapa, hakutakuwa na mtu wa kati,” alisema Zhang.

Alisema baada ya kukamilika kwa kituo hicho, wafanyabiashara watahitaji kuagiza bidhaa zao nje kupitia hapo na kuepuka gharama za usafiri, malazi na muda ambazo zitakuwa sio za lazima.

Meneja huyo huyo alisema kampuni yao itahakikisha watakuwa na majengo mapya na ya kisasa katika mita za mraba 90,000 ndani ya ghorofa nne.

Zhang alisema jengo hilo litakuwa na mwonekano wa kisasa na wa kuvutia na pia litabadili mandhari ya eneo la Kituo cha Mabasi cha Ubungo, ambacho hivi karibuni kitahamishiwa Mbezi.

Alisema kituo hicho kitakachokuwa namba moja katika eneo la Afrika Mashariki, kitakuwa na uwezo wa kuingiza watu 100,000 kwa siku na eneo la maegesho ya magari zaidi ya 1,000.

Zhang alisema katika kituo hicho kila duka litakuwa na ukubwa wa mita 15 za mraba na kwa watakaohitaji eneo kubwa zaidi ya hilo watatoa maelekezo na watategenezewa.

Alitaja biashara zitakazokuwapo kuwa ni za bidhaa za aina zote, kampuni za usafirishaji wa meli na ndege, mabenki, kampuni za mawakala wa usafirishaji, ofisi za viwanda vinavyotengeneza bidhaa za China na nchi nyingine duniani na nyingine zitakazojitokeza.

Zhang alisema pamoja na kuwapo kwa biashara za aina zote, huduma za Serikali ikiwamo ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA) na Idara ya Uhamiaji pia zitapatikana katika eneo hilo.

Alisema kampuni hiyo inatarajia kuuza maeneo ya biashara ambayo yatakuwa na maduka 2,600 hadi 2,800 kuanzia Januari mwakani (wiki moja ijayo) na wataendelea kwa miezi sita.

“Tutauza maeneo hayo ya maduka kuanzia Dola za Marekani 50,000 (Sh milioni 115.1) hadi Dola 100,000 (Sh milioni 230.1) ambapo mnunuzi atakuwa na haki ya umiliki kwa miaka 30,” alisema.

Zhang alisema pamoja na mauzo hayo, kwa siku zijazo kituo hicho kitakuwa rasmi kuhudumia wafanyabiashara wa Tanzania na wa nchi jirani za Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burundi ambao pia hawatahitaji kufuata bidhaa nje bali wataagiza kupitia Tanzania.

“Hiki kama nilivyoeleza kitakuwa kituo kikubwa cha biashara ya jumla na ya rejareja, kwa ajili ya kusambaza bidhaa kutoka nchi za mbali kwa nchi zote zinazopakana na Tanzania,” alisema.

Alieleza kuwa kitakuwa ni kituo kikubwa kuliko Mlimani City au Kariakoo ambako watu kutoka mikoani na nchi jirani hufika kununua bidhaa za biashara na kitakuwa ndicho kitovu cha biashara nchini na nchi zote jirani.

Alisema kwa sasa taarifa zote zinapatikana katika ofisi zao zilizopo kwenye jengo la Ubungo Plaza, ambako pia kuna sampuli ya namna kituo hicho kitakavyokuwa.

Kampuni ya Shanghai Ling Hang Group inayoendeleza eneo hilo, ina makao yake makuu mjini Shanghai, China na matawi nchini Singapore, Hong Kong, Dubai na sasa Tanzania.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,400FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles