29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Samia: Mchango wa mwanamke utambulike kiuchumi


Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, amesema sasa umefika wakati sera za uchumi wa nchi zitambue mchango wa mwanamke katika uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi wa taifa.

Amesema hatua hiyo inatokana na kuwa wanawake wengi wamekuwa wakishiriki kujenga uchumi kupitia sekta isiyo rasmi, lakini bado wamekuwa hawatambuliki kwenye sera.

Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam, alipokuwa akizundua akaunti maalumu ya wanawake kupitia Benki ya TPB.

Alisema hatua ya kuzinduliwa kwa mkakati huo ni njia mahsusi ya kumwezesha mwanamke aweze kufikia malengo yake.

Samia alisema Rais Dk. John Magufuli amesema amekuwa akiwathamini wanawake na ndiyo maana hata ilipofika hatua ya kufunga baadhi ya benki za Serikali ambazo zilikuwa zinajiendesha kwa harasa, aliamua iliyokuwa Benki ya Wanawake Tanzania ihamishiwe TPB ili kuenzi na kupata usimamizi mzuri wa masuala ya wanawake ikiwamo kuwa na huduma maalumu zinazowahusu.

“Benki ya TPB ipo imara na ndiyo maana katika utekelezaji wa agizo la Serikali wamehakikisha huduma zile zilizokuwa zinatolewa na Benki ya Wanawake sasa tunazikuta huku. Na kufunguliwa kwa akaunti maalumu ya Tabasamu ni sehemu ya kuenzi mchango wa wanawake nchini.

“Tunajua kwamba wanawake ndio wazalishaji wakubwa na ndio wenye kumiliki viwanda vidogo na vya kati, lakini bado mchango wao hautambuliki kwenye ukuaji wa uchumi. Na hili linaweza kuwa kwenye hata kwenye sera zetu, sasa wakati umefika Mheshimiwa Naibu Waziri Dk. Ashatu Kijaji, anzeni sasa kufanya marekebisho ya sera hizo ili kuweza kutambua mchango huu,” alisema Samia.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TPB, Dk. Edmund Mndolwa, alisema kuwa benki hiyo imefanya mabadiliko makubwa katika huduma ikiwamo kuwa na akaunti maalumu ikiwamo ya Tabasamu kwa lengo la kusogeza huduma bora kwa jamii.

“Kuzinduliwa kwa akaunti hii ya Tabasabu sasa kunakwenda kumfanya mwanamke kuwa sehemu ya uchumi wa nchi yetu kwa kuweza kupata huduma mbalimbali ikiwamo mikopo ya gharama nafuu na hili sasa linakwenda kuondoa fikra potofu kwa jamii,” alisema Dk. Mdolwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles