22.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Watoto wasilale na chuchu mdomoni – Daktari

GLORY LYAMUYA (DSJ) Na TUNU NASSOR

-DAR ES SALAAM

DAKTARI bingwa wa afya ya kinywa na meno kwa watoto wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Conrad Mselle  ameishauri jamii kuacha tabia ya kuwapeleka watoto kwa waganga wa jadi kwa madai ya kuwa na meno ya plastiki.

Pia ameshauri kutokumwacha mtoto alale na chuchu ya mama mdomoni hasa wakati wa usiku kwa kuwa bakteria wanaoishi mdomoni hutumia sukari kuzalisha tindikali inayosababisha meno kuvunjika.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Mselle alisema kitaalamu hakuna meno ya plastiki.

Alisema wazazi wa watoto wenye changamoto yoyote ya kinywa wanatakiwa kuwapeleka kwa daktari wa kinywa na meno kwa uchunguzi na matibabu na si tiba mbadala.

“Wasiwapeleke kwa waganga wa jadi ambako wamekuwa waking’olewa kwa kutumia vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ‘spoku’ za baiskeli jambo linalosababisha kupata maambukizi mbalimbali,” alisema Dk. Mselle.

Aidha alieleza kuwa hatua hiyo imekuwa ikiwasababishia watoto madhara makubwa kiafya, ikiwa ni pamoja na kutokwa damu nyingi.

Dk. Mselle alitolea mfano kuwa jamii nyingi za wafugaji wamekuwa wakitumia njia hiyo na kusababisha maumivu makali kwa watoto na hata wengine kupoteza maisha. 

“Niwashauri wazazi kusafisha vinywa vya watoto wao mara baada ya kuwapa dawa za maji (syrup) kwa kuwa kutokufanya hivyo bakteria huitumia kuzalisha tindikali na kuharibu meno,” alisema Dk. Mselle.

Alisema zaidi ya asilimia 50 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na tatizo hilo na kuwasababishia kushindwa kula.

Dk. Mselle alitoa wito kwa wazazi kuacha kuongeza sukari ya aina yoyote kwenye maziwa au vinywaji vingine vya mtoto kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha uharibifu wa meno.

“Wazazi wahakikishe watoto wao hawatumii sukari zaidi ya mara tano kwa siku ili kuepuka madhara ya meno,” alisema Dk. Mselle.

Aidha aliwashauri wachunguze afya za kinywa cha watoto wao angalau mara moja kwa mwaka kuanzia anapotimiza mwaka mmoja tangu kuzaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,057FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles