Ferdnanda Mbamila, Dar es Salaam
Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA), limempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi wake wa kurudisha kikokotoo cha zamani kiendelee kutumika kwani kitaleta tija kwa wafanyakazi.
Kabla ya Rais Magufuli kufikia uamuzi huo kanuni za Usimamizi wa Mifuko ya Jamii ziliondoa mfumo wa zamani wa kulipa asilimia 50 ya mafao kwa mkupuo na inayobaki kulipwa taratibu abapo mabadiliko yalitaka mstaafu alipwe alipwe asilimia 25 kwa mkupuo asilimia 75 itolewe kama pensheni kwa kila mwezi kwa kipindi chote cha maisha ya mstaafu jambo lililozua mijadala mbalimbali kuhusu jkanuni hizo mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamis Januari 3, jijini Dar es Salaam Dk. Yahaya Msigwa Naibu Katibu Mkuu TUCTA, Dk. Yahaya Msigwa amesema wanamshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuiweka sheria hiyo wazi kwa wafanyakazi ambapo inatarajia kufikia ukomo mwaka 2023.
“Rais ameweka sheria hiyo ili kuwapisha wadau mbalimbali nchini ili waje na sheria yenye tija na inayolinda maslahi ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi za jamii.
“Awali mifuko hiyo ilikuwa mitano na baada ya kuunganishwa sasa ipo miwili na ilitokana kubadilishwa kwa sheria hiyo, hivyo kwa namna moja imewarahisishia wadau wa mifuko hiyo kutoka katika mkanganyiko ambao uliwaweka gizani , “ amesema Dk. Msigwa .
Dk Msigwa ameitaja mifuko miwili ya jamii iliyopo baada ya kuunganishwa ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF ) na Mfuko wa Watumishi wa Sekta binafsi (NSSF).
Aidha mifuko mitano iliyokuwepo awali ni Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali Kuu (GEPF), Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa Serikali za Mitaa(LAPF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) na Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma na NSSF yenyewe.