30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wapinzani watua mahakamani

*Wafungua kesi kwa hati ya dharura kupinga muswada vyama vya siasa

*CCM yawabariki, yasema ni haki kidemokrasia, mahakama itaamua

ANDREW MSECHU,DAR ES SALAAM

VYAMA 10 vya upinzani nchini vimefungua kesi Mahakama Kuu kupinga kuwasilishwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa bungeni.

Kesi hiyo iliyofunguliwa Desemba 20, mwaka jana na viongozi wa vyama hivyo wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Joram Bashange, Salim Bimani na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, itaanza leo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Wakati wapinzani wakifungua kesi hiyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uamuzi huo ni mwema na ndiyo matakwa ya demokrasia na wana imani mahakama itatoa uamuzi kwa kuzingatia weledi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwa niaba ya viongozi wa vyama 10 vya siasa vilivyoungana katika suala hilo, Zitto alisema wameamua kufungua kesi hiyo kupinga muswada huo kujadiliwa na Bunge katika kikao chake cha Januari 29.

 “Waombaji katika kesi hiyo tumefungua maombi chini ya hati ya dharura Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam tukiiomba kutamka kuwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa unaokusudiwa kusomwa bungeni kwa mara ya pili wakati wa kikao kijacho cha Bunge mwezi Januari mwaka huu wa 2019, kuwa unakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) pamoja na marekebisho yake,” alisema Zitto.

Alisema kutokana na udharura huo, japokuwa mahakama iko likizo, lakini kesi hiyo iliyosajiliwa kwa namba Misc Civil Cause No.31/2018 imepangiwa kuanza kusikilizwa leo mbele ya jopo la majaji Sehel J, Magimbi J, & Masoud J na kusimamiwa na mawakili Mpare Kaba na Daimu Halfani watakaowasilisha hoja za walalamikaji.

Zitto alidai kwamba muswada huo unalenga kuisaidia CCM iliyochoka na kufilisika kuendelea kwa msaada wa dola na taasisi zake kwa kupata sheria kandamizi kwa minajili ya kufifisha ushindani wa kweli wa kisiasa unaotokana na nguvu tofauti kwa sababu vyama vya siasa hujijengea uwezo kwa kupambana kwa hoja.

“Tumeamua kufungua kesi hiyo kwa kuwa muswada huo ukisomwa na kuchambuliwa kwa ujumla wake, iwapo utajadiliwa na kupitishwa kuwa sheria, jambo ambalo linawezekana kutokana na wingi wa wabunge wa CCM ambao itikadi kwao ni zaidi ya masilahi mapana ya taifa, ni dhahiri sheria hiyo itanyang’anya uhuru, haki za msingi na kubinya haki za msingi,” alisema.

Zitto alisema muswada huo uliobeba mambo ambayo ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) kama ilivyorekebishwa katika ibara zake za 18, 20 na 21 ingawa ulipelekwa bungeni kusomwa kwa mara ya kwanza ikidaiwa kuwa unaboresha sheria iliyopo sasa ya vyama vya siasa, umetungwa kwa ajili ya kufifisha demokrasia nchini.

Alisema mapungufu ya wazi ni kufanywa kuwa jinai matendo yafanywayo na vyama vya siasa, kutoa madaraka makubwa kwa Msajili ya Vyama vya Siasa na kumpa kinga pamoja na watumishi wa ofisi yake dhidi ya mashtaka ya kuingilia uhuru wa vyama vya siasa kujiendesha.

Zitto alisema ni dhahiri kwamba muswada huo umeandaliwa kutekeleza tamko lililotolewa na Rais John Magufuli katika hotuba yake kwa wanachama wa CCM mkoani Singida mwaka 2016, alipozuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.

“Kwa sasa, tamko hilo pamoja na kuwa kinyume cha katiba na sheria za nchi, linaendelea kushikiwa bango na vyombo vya ulinzi na usalama kuwabana wapinzani wakati chama tawala kikiendelea na shughuli zake za kisiasa bila pingamizi lolote,” alisema.

Zitto alisema ni dhahiri kwamba muswada huo pia unalenga kumpa Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka ya usimamizi, hivyo kuwa na uwezo wa kuingilia shughuli za kiutawala na maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa ikiwemo kusimamisha na kufukuza uanachama.

“Tumeamua kupinga suala hilo mahakamani kabla muswada huo haujakabidhiwa rasmi kwa Bunge kwa kuwa ni wazi kutokana na utamaduni wa wabunge walio wengi wa CCM, ambao wamedhihirisha kuwa ‘makasuku’, pamoja na madhaifu yaliyopo, iwapo utafikishwa bungeni utapita na kuongezewa vipengele ambavyo vitafanya kupatikana kwa sheria mbaya kuliko ulivyo muswada wenyewe,” alisema.

Zitto alisema hata hivyo wapo wabunge wenye maana ndani ya CCM ambao wanazungumza nao, lakini wabunge ‘wapenda sifa’ wanadaiwa kuwa wana mpango wa kupeleka jedwali la marekebisho ili kuharibu zaidi muswada huo utakapofika bungeni.

Alisema kwa pamoja wanapinga muswada huo pamoja na maudhui yake kufikishwa na kujadiliwa bungeni, kwa kuwa japokuwa Serikali ndiyo inayoupeleka bungeni, lakini kwa mujibu wa taratibu ukishafikikishwa na kufikia hatua ya kujadiliwa, Serikali itajivua na kusema kuwa haina mamlaka katika muswada huo zaidi ya Bunge.

KAULI YA CCM

Kutokana na uamuzi huo wa wapinzani, MTANZANIA ilimtafuta Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga, ambaye  alisema hatua hiyo ni mwafaka kwa kuwa vyama hivyo vinatimiza matakwa na haki yao ya kidemokrasia.

Lubinga alisema ni kweli muswada huo umeandaliwa na Serikali inayoongozwa na CCM na umepitia hatua zote muhimu, kwahiyo kama wanaona kuna sehemu haki yao inakiukwa, mahakamani ni sehemu sahihi pia.

“Katika hili, CCM ndiyo inayoongoza Serikali na muswada huo ni sehemu ya Serikali. Kwahiyo kwa kuwa CCM siyo mahakama, tusubiri mahakama ina taratibu zake na itatoa maamuzi yake kwa kadiri itakavyoona inafaa,” alisema Lubinga.

Vyama 10 vinavyopinga muswada huo ni Chadema, ACT-Wazalendo, Chaumma, CUF, ADC, CCK, DP, NCCR-Mageuzi, NLD na UPDP.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles