24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Bashir kujiuzulu wadhifa wake?

KHARTOUM, SUDAN

UAMUZI wa Rais wa Sudan, Omar al-Bashir kumkabidhi uongozi wa chama tawala nchini humo makamu wake aliyeteuliwa hivi karibuni, Ahmed Harun, umetafsiriwa kuwa ni hatua ya pili ya kiongozi huyo aliyedumu kwa muda mrefu kung’atuka madarakani, huku maandamano yanayopinga serikali yake yakizidi kushamiri na wengine nane wakiwa wamefungwa jela kwa kosa hilo.

Duru za kisiasa zinasema kuwa, rais huyo alianza mchakato wa kujiuzulu mara baada ya kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi katika serikali yake.

Rais Bashir amemkabidhi uongozi Ahmed Harun kama Kaimu Mwenyekiti wa chama tawala nchini humo cha NCP hadi mkutano mkuu ujao wa chama utakapofanyika na rais mpya wa chama kuchaguliwa.

Awali Harun aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa NCP, wakati alipofanya mabadiliko makubwa kwenye serikali yake kwa lengo la kukabiliana na maandamano yanayoendelea.

Hata hivyo, makamu huyo mpya anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ya ICC iliyoko mjini The Hague, nchini Uholanzi, kwa makosa ya uhalifu wa kivita katika Jimbo la Darfur, kama ilivyo kwa Rais Bashir mwenyewe.

Chama cha NCP kina wingi wa viti bungeni na kwa mujibu wa kanuni zake, mkuu wa chama ndiye anakuwa na nafasi ya kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais, uliopangwa kufanyika mwaka 2020.

Sudan imekumbwa na maandamano makubwa yanayoipinga serikali ambapo waandamanaji nane wanaoipinga serikali wamehukumiwa kifungo cha jela juzi. Adhabu hiyo ni ya kwanza kutolewa na Mahakama maalumu ya dharura iliyoanzishwa na Rais Bashir ili kupambana na watu wanaomtaka ajiuzulu wadhifa wake.

Waandamanaji hao nane walikuwa ni miongoni mwa mamia waliomiminika mitaani katika miji ya Khartoum na Omdurman, wakikiuka katazo la kufanya maandamano yaliyoanza kwa mara ya kwanza Desemba mwaka jana juu ya kupanda gharama za maisha na tangu wakati huo yakapamba moto na kutoa shinikizo kubwa kwa utawala wa miongo mitatu wa Bashir.

Waziri Mkuu, Mohamed Tahir Ayala, aliyeapishwa hivi karibuni, amesema kuna jitihada za kushughulikia changamoto zilizopo.

“Nimejadiliana na rais kuhusu kazi inayotakiwa kufanyika na mazungumzo na vyama vyote vya siasa juu ya kuwa na mpangilio ambao utaweza kuanzisha serikali yenye ufanisi na iliyo na uwezo wa kushughulikia masuala ya kitaifa na kutimiza matakwa na matamanio ya watu,” alisema Waziri Mkuu.

Bashir si tu amepiga marufuku mikutano, bali pia amekabidhi mamlaka kwa vikosi vya usalama kufanya uvamizi na upekuzi binafsi kama sehemu ya hali ya dharura ya nchi nzima iliyotangazwa baada ya jaribio la kukabiliana na maandamano kushindwa.

Waandamanaji wamehukumiwa kifungo jela cha kati ya miezi sita hadi miaka mitano na mahakama tatu tofauti mjini Khartoum. Kwenye taarifa yake muungano wa mawakili wa demokrasia ambao ni sehemu ya kundi linaloongoza harakati dhidi ya utawala wa Bashir, umesema kuwa kiasi cha waandamanaji 870 walifikishwa mahakamani mjini Khartoum katika kipindi hicho cha hali ya dharura na katika mji pacha wa Omdurman.

Mamlaka zinasema jumla ya watu 31 wameuawa katika vurugu zinazohusiana na maandamano hadi hivi sasa, lakini shirika la Human Rights Watch linasema jumla ya watu 51 wameuawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles