25.4 C
Dar es Salaam
Thursday, January 9, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WAZIRI: IDADI YA TEMBO IMEONGEZEKA

Na UPENDO MOSHA -MOSHI


SERIKALI imesema idadi ya tembo katika hifadhi mbalimbali za Taifa na mapori ya akiba imeanza kuongezeka, baada ya juhudi za kupambana na ujangili uliokuwa unatishia usalama wa wanyama hao kupungua kwa kiasi kikubwa.

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini, Prof. Jumanne Maghembe, aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii (KILIFAIR), yanayofanyika kwa siku tatu katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika (MoCO), mjini hapa.

Waziri Maghembe alisema ujangili uliokuwa umeshamiri katika hifadhi mbalimbali za Taifa na mapori ya akiba umepungua kwa kiasi kikubwa, baada ya Serikali kupambana na majangili kwa nguvu zote.

“Tunaona tembo katika hifadhi zetu wameanza kuongezeka, hii ni kutokana na juhudi zetu za kupambana na ujangili kama serikali, kuzaa matunda,” alisema Waziri Maghembe.

Alisema licha ya mafanikio madogo kuonekana, Serikali inaendelea kujizatiti na kubuni mbinu mpya kila siku kwa lengo la kulinda na kupambana na ujangili.

Katika hatua nyingine, Waziri Maghembe alisema Serikali imejipanga kukuza utalii  kwa kuweka mikakati mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kushiriki maonyesho makubwa ya kimataifa ya utalii maeneo mbalimbali duniani.

“Tumejiwekea mikakati mbalimbali kwa lengo la kukuza utalii wetu hapa nchini, moja ya mikakati hiyo ni kutangaza vivutio vya Tanzania katika televisheni za nchi nyingine duniani, hii itasaidia kuongeza idadi ya wageni hapa kwetu,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilimanjaro Tourism & Fair (Kilifair), Dominic Shoo, alisema wamejipanga vema na kwamba katika maonyesho ya mwaka 2018 watajitahidi kuendelea kushirikisha watu mbalimbali kutoka katika mataifa yote duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles